KIZAAZAA MAFUTA TRA CHATUA TANGA, DOM

WIMBI la kubana vituo vya mafuta vinavyouza bidhaa hiyo bila kuwa na mashine za kutolea risiti (EFDs) za Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), limeingia kwa kishindo Dodoma na Tanga.

Kwa Dodoma, vituo 15 vilivyopo katika Manispaa hiyo vilifungwa jana na huko Tanga jumla ya vituo 18 navyo vilifungwa. Kwa upande wa Tanga, baadhi ya vituo ambavyo vilifungwa kutokana na kukosa mashine za EFDs ni TOC kilichopo Mtaa wa Donge, Ngamiani Petrol Station kilichopo Barabara ya 11, TAPCO kilichopo Mabanda ya Papa, STAR kilichopo Barabara ya Saba, Lake Oil kilichopo eneo la Reli na Afro Oil.

Kwa Dodoma, vituo vilivyofungwa ni vya makampuni ya TIOT, Ibra General Interprises, TSN, Oil Com (vituo 3), Camel Oil (vituo 2), Lake Oil (vituo 2), State Oil, GP 88 (vituo 2) na Afroil.

Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Thomas Masese alisema kuwa kazi hiyo wanaifanya kutekeleza matakwa ya sheria na kwamba wenye vituo walipewa muda wa kutosha kufunga mashine hizo, lakini hadi sasa hawajafunga.

Meneja huyo alisema kazi ya kukabiliana na watu wanaokiuka sheria ya kodi ni endelevu na kwamba hawataishia katika vituo vya mafuta pekee, bali na kwenye maeneo mengine ya biashara.

Akihojiwa, Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Vituo vya Mafuta Tanzania (TAPSOA) Kanda ya Kati, Faustine Mwakalinga alisema zoezi hilo linaweza kuleta madhara katika uchumi wa nchi kwa kuwa vituo vingi vya mafuta hasa vilivyoko kwenye wilaya mbalimbali, havijafungwa mashine hizo.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme aliyeambatana na maofisa wa TRA katika ukaguzi huo, aliwataka wafanyabiashara kutoa ushirikiano kwa kufuata kanuni za kodi za biashara zao. Alisema hasara inayotokana na uzembe au kukaidi maagizo ni kubwa na serikali haitamuonea aibu mtu ambaye anaendesha biashara kinyume na sheria.

Wakati huo huo, akizungumza na Habarileo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema TRA haitatoa muda wa majadiliano za ziada na wenye vituo vya kuuza mafuta, ambao wamekaidi kufunga mashine za kielektroniki kwenye pampu za kuuzia mafuta na kuwataka watii sheria na kufunga mashine hizo.

Aidha, alisema madai yanayotolewa na wamiliki wa vituo hivyo hayana msingi kwa sababu walishafanya makadiliano tangu mwaka jana na kupewa muda wa nyongeza ambao ni miezi mitatu, lakini hadi leo bado wamekaidi agizo hilo la kisheria.

“Kwanza tumechelewa sana kufanya uamuzi wa kuwafungia, tumekuwa na huruma kupita kiasi, walipaswa wawe wamefunga mashine hizo tangu Septemba mwaka jana, ila wamekaidi,” alisema.

Akifafanua majadiliano baina yao na wamiliki hao, Kayombo alisema, mapema mwaka jana, waziri wa fedha aliwapa wamiliki hao muda wa nyongeza kuanzia Julai 16 hadi Septemba 16, 2016 wawe wamefunga mashine hizo kwenye pampu za mafuta.

Hata hivyo agizo hilo halikutekelezwa kwa wengi wao isipokuwa kwa baadhi yao ambao ni pamoja na Puma, Total na Gapco waliotii na kufunga mashine hizo mapema. Alisema sheria ya kutumia mashine za EFD’s kwenye vituo vya mafuta ilitakiwa ianze kutekelezwa tangu mwaka 2014, lakini waliona ni busara kujadiliana na wauzaji hao na waziri akawapa tena muda wa miezi mitatu.

“Lakini cha kushangaza hadi leo wamekaidi, na tulinyamaza bila kuchukua hatua sasa tumeamua kuwafungia hadi pale watakapotekeleza sheria halali,” alisema Kayombo. Akizungumzia madai yanayotolewa na Chama cha Wamiliki Wauza Mafuta Rejareja (TASDOA) ,kuwa mashine hizo ni ghali na walikuwa kwenye mazungumzo na mamlaka hiyo, Kayombo alisema, madai hayo hayana msingi.

Alifafanua kuwa hivi sasa mashine moja ya EFD’s inafungwa kwenye pampu nne za mafuta hivyo kama kituo kina pampu nane mashine zinazohitajika kwenye kituo kizima ni mbili tu na kwamba wauzaji hao wanatafuta visingizio visivyo na sababu za msingi.

“Hakuna sababu ya msingi ya wao kutofunga mashine hizo, ukaidi hautowasaidia kitu, wanachotakiwa ni kufunga mashine hizo na kutoa risiti nah ii sio faida kwetu tu na kwao pia kwa sababu wanafanya biashara bila kujua kuwa na kumbukumbu,”alisema Kayombo.

Hivyo alisema uhakiki wa mashine hizo unaendelea kwa nchi nzima na kwamba kinachofanywa sio uhakiki kwenye vituo vya mafuta pekee bali ni kwa wafanyabiashara nchi nzima, hivyo wafanyabiashara wote wanapaswa kutumia mashine hizo. Na Sifa Lubasi (Dodoma), Anna Makange (Tanga) na Ikunda Erick (Dar).