Diwani Dar anaswa kwa rushwa mil 5/-

DIWANI wa Kata ya Msigani, Ubungo, Israel Mushi (48) na Mrasimu Ramani wa Manispaa ya Ubungo, Francis Mwanjela (28 ) wamekamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru) kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni 5.

Mkuu wa Takukuru katika Mkoa wa Kinondoni, Teddy Mngajira, alisema katika taarifa yake kuwa, watuhumiwa hao walikamatwa Jumatano wiki hii baada ya kupokea kiasi hicho cha pesa kutoka kwa mwananchi (jina limehifadhiwa) ambaye mbali ya kutoa kiasi hicho cha pesa, alitakiwa na watuhumiwa kuwapa rushwa ya Sh milioni 10.

Watuhumiwa wanadaiwa walishawishi na kupokea rushwa ili waweze kutoa ushawishi kwa wajumbe wa kamati ya mipango miji inayoshughulikia maombi ya kubadilisha michoro, kubadilisha matumizi ya kiwanja na kupitisha kibali cha ujenzi katika Manispaa ya Ubungo.

Uchunguzi wa tuhuma dhidi yao unaendelea na watuhumiwa wanaohusishwa kutenda makosa kinyume na Kifungu Namba 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007, wamepewa dhamana.

Aidha, Mngajira amewaasa viongozi wote wa umma, wanasiasa na watumishi wa umma, kuheshimu nyadhifa zao na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria bila kujihusisha na vitendo vya rushwa. Pia, ametoa mwito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Takukuru kuwafi chua wanaojihusisha na vitendo vya rushwa ili wachukuliwe hatua za kisheria.