‘Hatupo tayari kupokea misaada yenye masharti’

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan (pichani) amesema Taifa halipo tayari hata kidogo kupokea misaada yenye masharti, ambayo haiendani na mila na desturi za Kitanzania.

Alisema hayo jana baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu wa Ireland, Mary Robinson pamoja na Mwanzilishi wa Taasisi ya Graca Machel, Graca Machel na wajumbe walioambatana nao Ikulu, Dar es Salaam.

Alisema kuna baadhi ya wafadhili wanaisaidia Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na bajeti vizuri sana na bila masharti mabaya, lakini kuna baadhi ya wafadhili wanaonesha wazi kuwa wanataka Serikali ikubali masharti yao, ambayo yanaenda kinyume na maadili ya taifa, kitu ambacho hakiwezekani.