Urais wa Museveni wawatesa wabunge

URAIS wa kudumu unaopendekezwa nchini Uganda, umegeuka kuwa kero kwa wabunge, kiasi kwamba sasa wanaziogopa simu zao za mkononi.

Habari zilizopatikana zinasema wabunge wengi, wameamua kuzima simu zao za mkononi au kutozipokea pale wanapopigiwa, wakihofi a kukosolewa na kushutumiwa.

Wananchi walikuwa wakitaka wabunge wao, wasishiriki kubadili Katiba ya nchi kwa kuondoa Ibara Namba 102, inayoweka ukomo wa umri wa kugombea, ambapo mtu mwenye miaka 75 anazuiwa kuwania urais.

Kampeni hii inafanyika kwenye mitandao ya kijamii, ambapo nambari zote za simu za wanasiasa zimeorodheshwa. Kwa mujibu wa Katiba ya Uganda ya sasa, Rais Museveni hawezi kugombea tena urais.

Alianza kutawala mwaka 1986. Kiongozi wa Upinzani, Dk Kizza Besigye, aliwaonya wabunge kutokubali mchakato wowote wa kupiga kura kuhusu suala hilo. Aliwataka wafahamu kuwa “Rais Museveni na wafuasi wake wamejipanga kufanikisha hila hiyo”.

Hata hivyo, wanasiasa wa chama tawala cha NRM, wanaunga mkono kwa dhati hatua itakayomwezesha Museveni kugombea tena urais. Wanasiasa hao wana mtazamo kuwa katiba ni chombo hai, ambacho kimefanyiwa mageuzi mara kadhaa kulingana na hali ya kisiasa. Pia wanahoji kuwa “Ukomo wa umri si hoja katika mataifa mengi duniani kwa hivi sasa”.