Magufuli amlilia mke wa Mwakyembe

RAIS John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kutokana na kifo cha mkewe, Linah Mwakyembe aliyefariki dunia katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia jana.

Aidha, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana alifika nyumbani kwa Dk Mwakyembe, Kunduchi Beach jijini Dar es Salaam kuomboleza kifo cha Lina ambaye anatarajiwa kuzikwa keshokutwa wilayani Kyela mkoani Mbeya.Katika salamu hizo, Rais Magufuli alisema ameshtushwa na kusikitishwa kwa kifo hicho na hivyo yeye na familia yake wanaungana na familia ya Dk Mwakyembe katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

“Nakupa pole sana Dk Mwakyembe kwa kuondokewa na mkeo mpendwa Bi Linah, natambua hisia za maumivu ulizonazo wewe na familia nzima, nyote nawaombea Mwenyezi Mungu awatie nguvu, awape subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. “Namuombea marehemu Linah George Mwakyembe apumzishwe mahali pema peponi, Amina,” alisema Rais Magufuli katika salamu zake akiwa nyumbani kwake Chato mkoani Geita.

Kwa upande wake, msemaji wa familia ya Dk Mwakyembe, Solomon Kivuyo alisema Linah alikuwa akisumbuliwa na saratani ya titi kwa takribani miaka miwili. Kivuyo alisema familia ilijitahidi kadri ya uwezo wao kuokoa maisha yake kwa kumpeleka kimatibabu kwenye hospitali mbalimbali ndani na nje ya nchi. Alieleza kuwa Linah alipata matibabu kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na baadaye kupelekwa Aga Khan, India na Uturuki kabla ya kufariki dunia juzi kwenye Hospitali ya Aga Khan jijini.

Kuhusu utaratibu wa mazishi, msemaji huyo wa familia alisema kutakuwa na Ibada kesho saa 6.30 mchana kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Kunduchi Beach kabla ya mwili wa marehemu kupelekwa uwanja wa ndege saa 10 kwa kusafirishwa kwenda Kyela mkoani Mbeya kwa ajili ya maziko keshokutwa Jumatano. Aidha, msemaji wa familia hiyo alisema marehemu ameacha watoto watatu ambao ni George, Peter na Moses.

Mbali ya Waziri Mkuu Majaliwa, waombolezaji wengine waliofika nyumbani kwa Dk Mwakyembe kumpa pole na kumfariji, ni baadhi ya mawaziri wenzake, viongozi mbalimbali wengine wa serikali na wananchi wa kawaida. Wakati huo huo, Rais Magufuli amesali Ibada ya Jumapili ya 15 ya mwaka wa Kanisa iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato mkoani Geita na ameendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa hilo.

Katika harambee hiyo, Rais Magufuli ambaye aliongozana na mkewe, Mama Janeth Magufuli alifanikiwa kuchangisha Sh milioni 13, ahadi Sh 920,000, mifuko ya saruji 33 na malori 2 ya mchanga. Rais Magufuli aliwapongeza waumini wa Parokia ya Chato kwa hatua kubwa waliyopiga katika ujenzi wa kanisa kuu la Parokia hiyo na aliwataka kuendelea kujitolea kukamilisha hatua za mwisho za ujenzi huo.