UVCCM yamjia juu kigogo Chadema

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Arusha umesema kauli iliyotolewa na Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa ya kuwahusisha viongozi wa UVCCM na CCM kuwanunua madiwani wa Chadema waliojizulu, ni ya uongo.

Aidha, UVCCM imemtaka Golugwa kuthibitisha taarifa zake zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwa ushahidi, vinginevyo watachukua hatua kali dhidi yake.

Akisoma tamko la UVCCM Mkoa wa Arusha, Katibu wa umoja huo Mkoa, Said Goha mbele ya Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Mkoa na waandishi wa habari, alisisitiza CCM ni chama kikongwe hakijahusika na hakitahusika kwa namna yoyote ile kuwarubuni wadiwani wa upinzani kujiuzulu nafasi zao, bali wanafanya hivyo kwa utashi wao.

Goha alisema Chadema imesema mjumbe huyo ameoa binamu yake na katibu huyo wa Chadema Kanda ya Kaskazini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa. “Tunaomba amtaje kwa jina mke huyo na uthibitisho wa cheti cha ndoa au kielelezo chochote,” alisema.