Uuzwaji malighafi ya misitu waboreshwa

SERIKALI imeandaa utaratibu wa kuboresha uuzaji na ugawaji wa malighafi kutoka kwenye mashamba ya serikali ambapo hatua hiyo inalenga malighafi kutoka mashamba ya miti ya Misaji na miti kutoka mashamba mengine.

Ofisa Mawasiliano wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Tulizo Kilaga (pichani) alisema hayo jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa uuzaji huo kwenye mashamba ya Misaji utafanywa kwa njia ya mnada na makubaliano binafsi kama ilivyo sasa. Kilaga alisema kwa hatua hiyo, asilimia 30 ya malighafi iliyopangwa kuuzwa kwa mwaka itauzwa kwa njia ya mnada na njia hiyo itasaidia kubaini nguvu ya soko na kuongeza mapato.

Alisema kiasi kinachobaki ambacho ni asilimia 70 kitauzwa kwa makubaliano binafsi ili kutoa fursa kwa wadau wengi zaidi kushiriki kwenye biashara hiyo na kutoa fursa kwa wawekezaji wapya wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya misitu.

Aliongeza kuwa mgawo wa malighafi kutoka kwenye mashamba mengine ambayo inapatikana zaidi miti aina ya misindano, milingoti au misonobari utatolewa tu kwa wale wenye viwanda. Alisema katika kuboresha mahusiano na kuinua maisha ya jamii zinazopakana na misitu inayovunwa, vijiji vya pembezoni vitapewa mgawo.