RC atoa muda ukarabati mochwari

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stepen Kebwe amemtaka mkandarasi ambaye ni Wakala wa Majengo wa Serikali (TBA) kuongeza kasi ya ukarabati wa jengo la kuhifadhia maiti (mochwari) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ili ukamilike ndani ya wiki mbili zijazo.

Alisema hayo juzi alipofanya ziara kukagua maendeleo ya ukarabati huo baada ya kumalizika kwa zoezi la usafi wa eneo la hospitali hiyo. Awali, Mhandisi wa Idara ya Miundombinu ya Mkoa wa Morogoro, George Tarimo alisema katika Mwaka wa Fedha wa 2016/2017, Serikali mkoani humo kwenye bajeti ya maendeleo ya Mwaka wa Fedha wa 2016/2017, ilitenga Sh milioni 108.2 kwa ajili ya ukarabati huo.

Tarimo alisema ukarabati huo unasimamiwa na mshauri mwelezi na mkandarasi mkuu Ofisi ya Meneja wa Mkoa wa Wakala wa Majengo na ulianza Aprili 5, mwaka huu na kutakiwa kukamilishwa ifikapo leo. Alisema hadi sasa gharama za ujenzi ya awali ni Sh 89,602,993 na kwamba kiwango cha kazi zilizokamilika kimefikia asilimia 65. Alisema hiyo inatokana na nafasi finyu ya utendaji. Alifahamisha kuwa, jokofu lenye uwezo wa kuhifadhi miili 18 limenunuliwa na bado lipo Bohari kuu ya Dawa (MSD).