‘Ni mapambano ya rushwa, ukiritimba’

SERIKALI imeahidi kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa na ukiritimba kwenye mamlaka zinazohusiana na uwekezaji nchini ili kuwavutia wawekezaji zaidi hususani kutokea nchini China, hatua iliyotajwa kuwa itaongeza kasi zaidi kwenye uwekezaji kwenye sekta ya viwanda nchini.

Akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Sita wa Mwaka wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango (pichani) aliyemwakilisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu, alisema ni vigumu kwa serikali kufanikisha azma yake ya kufikia uchumi wa viwanda ikiwa vitendo vya rushwa na ukiritimba vitakithiri kwenye mamlaka zinazohusika na uwekezaji nchini.

“Nia hasa ni kunufaika na fursa za kiuwekezaji kutoka mataifa makubwa ikiwemo China ambao kimsingi wamekuwa washirika wetu kwa miaka mingi. Hata hivyo, tunaamini kuwa kama taifa, bado tunahitaji kunufaika zaidi na uwekezaji kutoka China na ndiyo maana tunaweka msisitizo zaidi katika kukabiliana na kila aina ya changamoto inayoweza kukwamisha unufaikaji huo ikiwemo rushwa na ukiritimba kwenye mamlaka zetu za kiuwekezaji,” alieleza Dk Mpango.