Mikoa 13 yakamilisha udadisi wa kaya

KAZI ya kuorodhesha kaya kwa ajili ya Utafi ti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18, inaendelea nchi nzima ikiwa ni maandalizi ya utafi ti huo unaotarajia kufanyika hivi karibuni.

Akizungumzia kazi hiyo, Meneja wa Takwimu za Jamii na Watu, Sylvia Meku wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) amesema mpaka sasa mikoa 13 imekamilisha kazi hiyo ambapo ni sawa na asilimia 50. “Zoezi la kuorodhesha kaya kwa ajili ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18 linaendelea vizuri na mpaka sasa wadadisi wamekamilisha kuorodhesha kaya katika mikoa 13,” alieleza Meku.

Aliitaja mikoa iliyokamilisha uorodheshaji wa kaya kuwa ni Dar es Salaam, Arusha, Manyara, Iringa, Njombe, Morogoro, Mwanza, Tabora, Katavi, Mbeya, Mara, Kagera na Lindi. Kazi ya uorodheshaji wa kaya inafanyika mikoa yote ya Tanzania Bara na inatarajia kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.

Utafiti kama huu mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2011/12 ambao ulionesha kuwa asilimia 28.2 ya Watanzania wanaishi chini ya mstari wa Umasikini wa mahitaji ya Msingi.

Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18 unafanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na baadhi ya Wadau wa Maendeleo kwa lengo la kupata viashiria vya kupima hali ya umaskini nchini.