Uhuru achuana vikali na Raila

WANANCHI wa Kenya milioni 19.6 waliojiandikisha kupiga kura kumchagua rais, wabunge, maseneta na magavana watakaowaongoza kwa miaka minne, wametekeleza haki yao hiyo ya kidemokrasia kwa kupiga kura kwa amani na utulivu katika maeneo mengi nchini humo.

Miongoni mwa watu mashuhuri waliojitokeza kupiga kura jana katika vituo vya kupigia kura 40,883 vilivyoidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) ni Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee, anayetetea kiti hicho, pamoja na Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, anayegombea urais kwa tiketi ya Muungano wa Vyama Vya Upinzani (Nasa).

Habari zilizopatikana baadaye jana usiku, zilieleza kuwa Kenyatta na Odinga walikuwa wakichuana vikali kwenye vituo vilivyomaliza kuhesabu kura, ambapo katika kura 1,571,000 zilizohesabiwa hadi wakati huo, Uhuru alikuwa amepata kura 904,477 wakati Raila alikuwa amepata kura 656,293. Jumla ya Wakenya milioni 19.7 walitarajiwa kupiga kura.

Kura zilianza kuhesabiwa jana jioni, muda mfupi baada ya kumalizika kwa upigaji kura na inatarajiwa kuwa matokeo yote, yataweza kutangazwa ndani ya wiki moja. Kwa mujibu wa historia za wagombea hao wa urais, Odinga aliyepiga kura katika kituo cha Shule ya Msingi Old Kibera, kwenye jimbo la Kibera, amewania nafasi hiyo kwa mara ya nne sasa, ambapo mara ya kwanza aligombea mwaka 1997 na kushindwa, mwaka 2007 aligombea tena na kuangushwa na akajaribu tena kwa mara ya tatu mwaka 2013 na kukosa kiti hicho.

Uhuru aliyepiga kura katika Shule ya Msingi Mutomo iliyopo Gatundu Kusini kwenye jimbo la Kiambu, alizungumza na wanahabari punde baada ya kutekeleza haki yake ya kupiga kura na kuwataka wananchi wa Kenya waendelee kudumisha utulivu na amani walioionesha mapema walipoanza kupiga kura, ili wayafurahie maisha sasa na baada ya uchaguzi.

“Hadi muda huu ninapomaliza kupiga kura, mambo yamekwenda vizuri, amani na utulivu vimetawala katika maeneo mengi ya nchi yetu. Ninasisitiza amani, amani, amani kwa Wakenya, kwa sababu hata baada ya uchaguzi kuna maisha na Kenya itaendelea kuwepo ikihitaji kuwa na watu,” alisema Uhuru. Kutokana na maelezo yake, jambo la msingi analoliomba hasa katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu ni amani itakayochochewa na viongozi wanaogombea nafasi mbalimbali kwenye kinyang’anyiro hicho kutokubali kuwa sababu ya vurugu na mapigano kwa kukataa matokeo.

Uhuru alisema hata ikitangazwa na Tume ya Uchaguzi kuwa ameshindwa, atakubali matokeo kwa moyo mweupe kwa kuwa anaamini utakuwa ndiyo uamuzi wa wananchi waliopiga kura. “Hivyo ndivyo ninavyotaka wagombea wenzangu wa nafasi mbalimbali za uongozi wafanye hasa mgombea urais kupitia vyama vya upinzani,” alisema. Mkewe Margareth Kenyatta alipiga kura katika kituo cha St. Mary’s High School kilichopo Nairobi, baada ya kukaa kwenye foleni kwa saa nne, wakati Naibu Rais William Ruto, pamoja na mkewe Rachel Ruto walipiga kura kwenye Shule ya Msingi Kosachei iliyopo Sugoi-Uasin Gishu.

Aidha, mgombea mwenza wa Odinga, Kalonzo Musyoka, alipiga kura katika kituo kilichopo kwenye Shule ya Msingi Tseikuru iliyopo Mwingi jimboni Kitui. Mgombea Urais akwama Mgombea mwingine wa urais, Dk Ekuru Aukot aliye miongoni mwa wagombea saba waliopania kumng’oa Uhuru madarakani kupitia uchaguzi huo, alijikuta katika wakati mgumu kwa saa kadhaa wakati alipotaka kwenda kupiga kura kwenye kituo cha Kapedo jimboni Turkana, baada ya kukosa pa kupita kutokana na mto Nginyag kufurika na kusababisha barabara zisipitike.

Tume ya Uchaguzi ililazimika kutafuta helkopta ili kuhakikisha vifaa vya uchaguzi, vinafikishwa katika vituo vilivyopo kwenye maeneo yaliyoathiriwa na mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha. Hilo ni miongoni mwa maeneo ambayo wapiga kura walichelewa kuanza kupiga kura, hata baada ya saa 06:00 za mchana. Mwitikio Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alisema mamilioni ya wananchi wa Kenya, wanaokadiriwa kuwa si chini ya asilimia 80 ya waliojiandikisha, walijitokeza kupiga kura.

Kupitia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakioneshwa moja kwa moja na televisheni tofauti za Kenya jana wakati wa kupiga kura, alionekana mwanamume aliyetambulishwa kuwa ni John Nyakundi (53), aliyejitokeza kupiga kura katika Shule ya Msingi Dandora iliyoko Nairobi, licha ya kuwa na tatizo la mapafu lililosababisha afike kituoni na mtungi wa oxygen aliyokuwa akiivuta kwa kutumia mipira maalumu.

Ilielezwa kuwa, kwa hali ya kawaida, mgonjwa kama Nyakundi anayesumbuliwa na ugonjwa wa mapafu kwa miaka miwili sasa, angeweza kuamua kukaa nyumbani, lakini aliamua kwenda kupata haki yake akiwa na mtungi wake wa gesi na mipira puani. Pamoja na Nyakundi aliyetolewa hospitali ili kupiga kura, wafungwa 5528 waliojiandikisha kupiga kura kutoka katika magereza 118 ya nchini humo nao walipiga kura. Hiyo inaelezwa kufanikishwa baada ya ombi waliowahi kulifikisha mahakamani kutaka wapewe haki ya kumchagua angalau rais wa nchi yao katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kukubaliwa.

Mbali na hayo, Mwenyekiti wa Tume hiyo ya Uchaguzi alisema katika ufuatiliaji wao walibaini vituo vingi vya kupigia kura vilifunguliwa kwa wakati unaotakiwa, ingawa kulikuwa na vichache vilivyochelewa kufunguliwa au kufunguliwa mapema na upigaji kura kuchelewa kuanza, kwa sababu ya uzembe wa wasimamizi, ambao hata hivyo, Tume hiyo ya Uchaguzi iliwachukulia hatua.

Alieleza kuwa kila kituo kati ya vituo vya kupigia kura 40,883 kilikuwa na uwezo wa kuhudumia wapiga kura 700. Wasimamizi waliozembea Kutokana na malalamiko yaliyotolewa kwa Tume na baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi na wapiga kura wengine kwenye maeneo yaliyochelewa kuanza upigaji kura, Mwenyekiti wa IEBC alisema waliamua kuwachukulia hatua wasimamizi kwa kuwaondoa katika kazi hiyo mara moja baada ya kubaini uzembe wao.

“Tumewaondoa wasimamizi watatu katika Jimbo la Nairobi ambao walikuwa kwenye maeneo ya kupigia kura ya Embakasi Mashariki, Kasarani na Westlands kwa sababu walichelewa kuanza kupigisha watu kura hadi walipokwenda kusimamiwa na Makamishna wa Tume ya Uchaguzi,” Chebukati alisema. Vilevile, alisema wamechukua hatua kadhaa kumaliza changamoto zilizojitokeza kwenye mashine za kupigia kura za kielektroniki (BVR) hasa zilizoshindwa kutambua watu, kwa kuzibadilisha na kuweka nyingine zilizofanya kazi vizuri.

Pia alisema walitumia helkopta kuwahisha karatasi za kura mahali paliposhindwa kupitika kama vile Turkana pamoja na kutoa msimamo kwa vituo vilivyochelewa kufunguliwa asubuhi kuwa viongeze muda kama uliopotea pindi vilipokuwa vimefungwa, baada ya saa za kupiga kura kwisha saa 11:00 jioni ya jana. “Hiyo itawezesha watu waliofika vituoni kupiga kura na kucheleweshwa na wapiga kura au sababu zinazoeleweka, kupata muda wa kutosha kupiga kura baada ya ule tulioupanga kumalizika. Huu ndiyo msimamo wa Tume,” alisema.

Watoto watumika Kufuatia ujanja wa baadhi ya watu waliokuwa wakiharibu foleni kwa sababu ya kutaka kuhudumiwa huku wakiwa wamechelewa kwa visingizio vya kuwa na watoto wadogo, wasimamizi wa kura katika vituo ambako ujanja huo ulibainika waliamua kuwaweka watoto alama ndogo vidoleni ili wasitumike vibaya. Taarifa zilizorushwa na televisheni za Kenya wakati kura zikipigwa kwenye jimbo la Homa Bay, zilisema kuwa badhi ya watoto walitumika zaidi ya mara moja kama kisingizio cha wanawake kwa wanaume kutaka kuhudumiwa nje ya mistari.

Maboksi ya kura yachanganywa Ilibainika kuwa boksi lenye karatasi za kura lililotakiwa kupelekwa katika Jimbo la Ndia katika mkoa wa Kirinyaga zilipelekwa kwa makosa na kupokelewa kwenye kituo kingine cha kura jana na kusababisha Polisi pamoja na maofisa wa IEBC kutumia helkopta kulifuata katika Shule ya Elimu ya Juu ya Sekondari ya Nakuru.

Waangalizi wa kimataifa Waangalizi wa Kimataifa walitembelea Gereza Kuu la Kenya na kuona upigaji kura ukiendelea, ambapo mmoja wao, Thabo Mbeki aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini alitoa pongezi kwa Kenya kuruhusu wafungwa wapige kura kumchagua Rais wa nchi yao. Mbeki alisema hiyo ni hatua ya kuigwa na mataifa mengine kwa sababu imezingatia misingi ya demokrasia na haki za kila raia wa Kenya hata kama ni mfungwa.

Alisema pia wameshuhudia uchaguzi ukiwa wa amani na utulivu katika maeneo mbalimbali waliyofanikiwa kufika, licha ya kuwepo na kasoro ndogo za kawaida ambazo Tume ya Uchaguzi ilifanya liwezekanalo kuzitatua kwa haraka. Kura zilianza kuhesabiwa jana jioni muda mfupi baada ya kumalizika kwa upigaji kura huo na inatarajiwa kuwa matokeo yote yataweza kutangazwa ndani ya wiki moja.