Samia: Wakulima nendeni mkakope

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu amewataka wakulima waache unyonge na kulalamika kuhusu kutokopeshwa na taasisi za kifedha na benki. Badala yake, amewataka waende kwenye Benki ya Wakulima iliyoanzishwa na serikali, wakakope kwa kuwa ni benki iliyoanzishwa kwa ajili ya kuwainua wao kiuchumi.

Akihutubia wakati wa kilele cha Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Ngongo mkoani hapa, Samia alisema serikali imeianzisha na kuweka mtaji mkubwa katika benki hiyo ili wakulima wakopeshwe na hivyo alitaka wakakope kwenye taasisi hiyo mpya. Alisema hadi sasa hivi wakulima wapatao 45,000 tu, ndiyo ambao wameshakopeshwa Sh bilioni 7.4.

“Hiki ni kiasi kidogo, nendeni mkapate mikopo mlime kwa ajili ya malighafi za viwanda,” alisema Makamu wa Rais. Kwa upande wa uhakika wa chakula, aliwataka wakulima kuhakikisha kwamba wanahifadhi chakula cha kuwatosha kwa mwaka mzima na kuuza ziada. Alisema katu Serikali haitatoa chakula kwa wilaya, ambazo zimepatwa na njaa kwa sababu ya uzembe wa watu.

“Huu ndiyo msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano, tutatoa msaada tu kwa wilaya ambazo zimepatwa na majanga ya asili, lakini kwenye uzembe mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa na wahusika wa kilimo watawajibika,” alibainisha Makamu wa Rais. Alisisitiza wananchi kufanya kazi kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuondokana na umasikini. Alisema Tanzania haina mjomba wa kuisaidia kwani wamewahi kutoa misaada miaka ya nyuma na hiyo misaada haikusaidia nchi kuondokana na umasikini. “Naomba mfanye kazi kwa bidii, tushikamane tufanye kazi ili tuweze kujitosheleza kwa chakula na tuijenge nchi yetu,” alieleza.

Akizungumzia miaka minne ya Maonesho ya Nanenane kufanyika kitaifa katika mikoa ya Kusini, Samia alisema kwamba miaka hiyo ni darasa tosha kwa wakulima, wafugaji na wavuvi. Alisema alishiriki mwaka jana na mwaka huu ameona mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo. Aliwataka wakulima waongeze jitihada katika ufufuaji na uwekezaji wa viwanda vipya.

Alisema fedha za mazao yao ya korosho ni fedha nyingi, zikitumika vyema zitabadili maisha ya wakulima wa mikoa ya kusini. Alisisitiza wakulima kulima kilimo cha biashara ili ujenzi wa viwanda ambao unapigiwa debe na serikali ukuta upatikanaji wa malighafi za mazao uwe wa uhakika kwa ajili ya viwanda husika. Alisema amezunguka mabanda mengi na kuona kwamba kiwango cha teknolojia, kimeongezeka. Aliahidi kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili wakulima wazalishe kwa wingi zaidi kwa kutumia teknolojia.

“Katika banda la Benki ya Kilimo nimeona namna wakulima wanavyopata mikopo, wanaelimishwa jinsi ya kutafuta masoko, nawaagiza limeni kwa bidii serikali inawatafutia masoko, tukifanikiwa kwa ajili ya soko la ndani na nje tutapata fedha za kigeni,” alisema Samia. Pia alisema kwamba serikali itahakikisha kwamba kila Mtanzania atanufaika na fursa zilizopo nchini ikiwemo kuendelea kupunguza tozo ada na kupunguza ushuru wa mazao.

Pia alipiga marufuku utozaji wa ada kwa mazao yanayotoka halmashauri moja kwenda halmashauri nyingine. “Ushuru unatozwa katika halmashauri yanakotoka mazao na siyo kila halmashauri yanakoingia, tutaendelea kuboresha mazingira ili kila mmoja anufaike na nchi hii,” alisema. Aliviagiza vyombo vya sheria kuanza uchunguzi dhidi ya wazabuni wote wa pembejeo, waliohusika kufanya udanganyifu kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia isiyo halali. Alisema serikali imepokea taarifa inayoonesha kuwa wazabuni wa pembejeo, wamefanya ubadhirifu mkubwa na hivyo jambo hilo siyo la kufumbiwa macho.

“Serikali imekamilisha utafiti wa madeni ya wazabuni wa pembejeo na hapa niseme, baada ya taarifa kukamilika hali siyo nzuri, tumegundua kiasi kikubwa cha udanganyifu,” alisema. Aliongeza “kuna ubadhilifu mkubwa uliofanywa pamoja na mbinu nyingi zilizotumika kujipatia fedha wakati pembejeo haikuwafikia wakulima.” Alisema kamwe Serikali ya Awamu ya Tano, haiwezi kulinda wahujumu uchumi wa taifa na wale wote waliohusika kuhujumu wakulima. Alisisitiza kuwa lazima hatua zichukuliwe na alimwagiza Waziri wa Fedha, kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa dhidi ya wote waliohusika.