Wilaya Songea hatarini kugeuka jangwa

WILAYA ya Songea mkoani Ruvuma inakabiliwa na tishio la kugeuka jangwa kutokana na wananchi kukata miti, kuchoma misitu moto na baadhi ya watumishi wasiokuwa waadilifu kuruhusu wafugaji kutoka mikoa mbalimbali nchini kuingiza idadi kubwa ya mifugo bila kufuata sheria.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Polole Mgema wakati akitoa salamu za serikali katika kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Wilaya ya Songea kilichofanyika katika Kijiji cha Lundusi katika Kata ya Maposeni.

“Kuna uharibifu mkubwa katika mlima Lihanje na nimekuwa nikitoa maagizo kwa watendaji wetu mara kwa mara kusitisha shughuli za kilimo katika mlima ule, hata hivyo bado imeonekana baadhi ya wananchi wanaendelea kukata miti na kufanya shughuli zao za kibinadamu,” alisema Mgema na kuongeza: “Kuna watumishi ambao ni wagumu sana kutekeleza maagizo ya serikali sasa mimi mwenyewe nitaanza operesheni ya kuwaondoa ndugu zenu, lakini msije kunilaumu kwa hatua nitakayochukua.”

Kwa mujibu wake, ataanza kupita kijiji hadi kijiji kwa ajili ya kuwatangazia wananchi kuhusu mpango wa serikali kutunza mlima Lihanje kutokana na umuhimu wake baada ya kuona watumishi waliopewa dhamana ya kusimamia uhifadhi wa mazingira katika mlima huo kushindwa kutimiza wajibu wao kwa sababu wanazozijua. Aidha, amewataka watumishi na madiwani kusimamia vema agizo la serikali la kutoruhusu uingizaji mifugo kutoka mikoa mingine na kuzuia biashara ya mkaa kwenda nje ya Wilaya ya Songea.