Bill Gates atoa mabilioni nchini

TAASISI ya Bill and Mellinda Gates imetenga Dola za Marekani milioni 350 (takriban Sh bilioni 777.084) kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya kilimo, afya na mifumo ya kielektroniki ya upatikanaji wa taarifa.

Wakati Bill and Mellinda Gates wakitenga fedha hizo, Serikali ya Marekani itatoa fedha za nyongeza kiasi cha Dola milioni 225 (Sh bilioni 499.500) katika mwaka ujao kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo itakayogusa sekta za elimu, afya, lishe bora, utawala bora. Hayo yalibainika jana wakati Rais John Magufuli alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti Mwenza wa Taasisi ya Bill and Melinda Gates, Bill Gates na baadaye katika mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dk Inmi Patterson.

Kwa upande wake, Gates alisema kama ambavyo taasisi yake imeshirikiana na Tanzania kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha huduma za afya nchini, fedha hizo zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi zaidi ya afya ikiwemo kupunguza vifo vya uzazi, kukabiliana na ugonjwa wa malaria, kuimarisha lishe na kukabili utapiamlo; katika sekta ya kilimo zitasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao, kuzalisha mbegu bora na kuboresha ufugaji utakaoongeza chakula na pia kuweka mifumo ya kisasa ya upatikanaji wa taarifa.

Tajiri huyo wa pili duniani alieleza kufurahishwa na maendeleo ya uchumi wa Tanzania pamoja na uongozi na msimamo wa Rais Magufuli juu ya kutaka miradi hiyo ilete matokeo yenye manufaa, na alisema atakuja Tanzania mara nyingi ili kuimarisha zaidi ushirikiano na kufuatilia utekelezaji wa miradi. Dk Magufuli alimshukuru Bill Gates kwa mchango mkubwa unaotolewa na Taasisi ya Bill and Mellinda Gates katika miradi mbalimbali nchini ikiwemo fedha ambazo taasisi hiyo itazitoa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa na amemhakikishia kuwa serikali yake itahakikisha fedha hizo zinaleta matokeo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dk Patterson alisema Marekani itatoa fedha za nyongeza kiasi cha Dola milioni 225 (Sh bilioni 499.500) katika mwaka ujao kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo itakayogusa sekta za elimu, afya, lishe bora, utawala bora. Dk Patterson alisema Marekani imeongeza fedha hizo katika miradi inayotekelezwa nchini kwa sababu ina dhamira ya dhati ya kushirikiana na Tanzania na itahakikisha uhusiano na ushirikiano huu unaendelezwa na kukuzwa zaidi.

Rais Magufuli alimshukuru Balozi Patterson kwa mchango mkubwa ambao Marekani imekuwa ikiutoa kwa Tanzania na alimhakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano wake na Marekani, na pia alimuomba awahimize wafanyabiashara na wawekezaji wengi zaidi wa Marekani, waje kuwekeza na kufanya biashara hapa nchini kutokana na fursa lukuki zilizopo.

Pia aliiomba Marekani kusaidia kujenga hospitali kubwa ya kitaifa katika makao makuu ya nchi mkoani Dodoma ili kuongeza uwezo wa mkoa huo kutoa huduma za matibabu ikilinganishwa na ilivyo hizi sasa. Mapema jana asubuhi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene kwa kushirikiana na Bill Gates, walizindua Mpango Shirikishi wa Taarifa za Afya nchini utakaogharimu Dola za Marekani milioni 75.

Uzinduzi huo uliohudhuriwa na wadau mbalimbali wa afya, ulifanyika Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam ukiwa ni Mpango wa Pili baada ya ule wa mwaka 2015 kumalizika. Waziri Ummy alisema kati ya dola milioni 75 za mpango huo, Mfuko wa Bill na Melinda Gates umechangia Dola za Marekani milioni 15. Imeelezwa kuwa katika awamu ya kwanza, mfuko huo ulichangia dola za Marekani milioni 1.6. Waziri Ummy aliwaomba wadau wengine, kujitokeza kuchangia ili kuufanikisha mpango huo wa miaka mitano.

Alisema lengo la Mpango huo ni kuimarisha mifumo ya taarifa za afya nchini kutolewa kwa njia ya kielektroniki ili kuondokana na matumizi ya vitabu au mafaili. “Upatikanaji wa taarifa kwa mfumo wa kielektroniki utatusaidia kujua namna huduma za afya zinavyotolewa kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa hadi taifa.

Itatuwezesha kufuatilia watoa huduma za afya nchini kwa kujua utendaji wao, idadi yao na idadi ya wagonjwa wanaowahudumia,” alieleza Ummy. Aliongeza kuwa mfumo wa huo wa kielektroniki pia utawasaidia kupata taarifa za vifo vinavyotokana na uzazi, kiasi cha dawa kinachohitajika na matumizi kwa kila hospitali au kituo cha afya, kupata taarifa za wagonjwa ili Serikali iweze kutoa huduma nzuri za afya. Kwa mujibu wake, ubora wa taarifa na matumizi bora ya taarifa ndiyo msingi wa kuwa na mfumo wa afya wenye ufanisi.

Alisema Mpango Shirikikishi wa Taarifa utasaidia katika kutekeleza mpango wa uwekezaji katika afya kielektroniki ulioandaliwa na kuidhinishwa kwa pamoja kati ya wadau zaidi ya 80 wa serikali na washirika wa maendeleo mjini Dodoma mwaka jana. Naye Simbachawene alisema mfumo huo wa upatikanaji wa taarifa kielektroniki, pia utaisaidia serikali kufuatilia fedha inazopeleka kweye vituo vya kutolea huduma kama vile zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa.

Alisema ni vigumu kudhibiti matumizi ya fedha hizo bila kuwa na mfumo madhubuti wa upatikanaji wa taarifa. Alisema serikali imeajiri wahasibu 500 kwenye vituo hivyo ili kuongeza uwazi, kujua matumizi ya fedha na kujua matumizi sahihi ya dawa. “Mfumo huu utaleta mapinduzi katika utoaji wa huduma za afya. Nawaomba Watanzania tuamke na tuchangamkie huduma bora za afya kwa kujiunga kwenye mifuko ya bima ya afya kama CHF hasa kwa wananchi wa vijijini na kwa kufanya hivyo serikali itapata fedha na kudhibiti upotevu wa fedha,” alisema Simbachawene.

Kwa upande wake, Bill Gates alisema mfuko wake unaamini kuwa ufanisi katika matumizi ya taarifa (data) ni muhimu katika kujenga mifumo ya afya iliyo imara. Alisema amekuja kujifunza vipaumbele vya kimaendeleo nchini ikiwemo matumizi ya taarifa na teknolojia katika kuboresha mifumo ya afya. Imeelezwa kuwa mfumo wa kielektroniki umetumika katika mikoa ya Tanga na Arusha na kusaidia kuwasajili watoto 85,000 ambao taarifa zao kuhusu chanjo zimepatikana na kuhifadhiwa kwa usahihi. “Mfumo umetusaidia kujua idadi ya watoto, chanjo ya ngapi anatakiwa kupata, majina yao, kiasi cha chanjo tulichonacho, lakini pia tumeweza kupata taarifa za wazazi. Kwa kupitia mfumo huu, mtoto anaposajiliwa tu, mtoa chanjo naye anapata taarifa hiyo wakati huo huo,” alieleza Millen Nkuzi ambaye ni Muuguzi Mkunga kutoka Tanga.