AU, Marekani wasifu uchaguzi wa Kenya

WAKATI Uhuru Kenyatta akiendelea kung’ara katika matokeo ya Urais ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Jumanne wiki hii, waangalizi wa kimataifa wamesifu uchaguzi huo, wakisema kwa kiasi kikubwa ulifuata taratibu.

Waangalizi hao kutoka Marekani, Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Madola walitoa ripoti yao ya awali kuhusu Uchaguzi wa Kenya na mazungumzo yao na Kambi ya Muungano wa Vyama vya Upinzani (NASA) waliokuwa wamewasilisha kilio chao cha kukosa imani na mfumo wa kielektroniki wa kupokea matokeo wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya.

John Kerry, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeongoza waangalizi wote wa kimataifa katika uchaguzi wa mwaka huu nchini Kenya, aliisifu IEBC kwa kuandaa uchaguzi mzuri uliotawaliwa na uwazi, huku akiwashauri NASA kufuata njia sahihi za kupinga matokeo kisheria, wakiwa na ushahidi wa maeneo yenye dosari. “Katika kituo kimoja nilishuhudia mama mmoja (ofisa wa IEBC) akiita watu kushuhudia anavyoingiza matokeo ya kura katika kompyuta… huu ni uwazi wa aina yake,” alisema Kerry aliyekiri kukutana na ujumbe wa NASA na mgombea wake wa urais, Raila Odinga, walilalamikia kuwapo kwa dalili za `rafu za uchaguzi’.

Naye Kiongozi wa Ujumbe wa Waangalizi wa AU, Thabo Mbeki ambaye ni rais wa zamani wa Afrika Kusini, alisema baada ya kukutana na ujumbe wa NASA, waliwaeleza kuwa kazi yao ni kuchunguza, hivyo kilio chao kitafikishwa EIBC. Rais wa zamani wa Ghana anayeongoza waangalizi kutoka Jumuiya ya Madola, John Mahama pia alisifu uchaguzi huo, huku akiwashauri NASA kuonesha ukomavu wa kisiasa na kwamba kama kuna dosari, wafuate njia sahihi kuzifichua.

Wakati waangalizi hao wakiyasema hayo, IEBC imekiri kulikuwa na njama za kufanya udukuzi katika mfumo wa kielektroniki wa kupokea matokeo ya uchaguzi wa tume hiyo, lakini hazikufanikiwa. Kamishna anayesimamia Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa IEBC, Yakub Guliye alisema jana na kuongeza kuwa, kila kitu kipo sawa, kwani wadukuzi hawakufanikiwa kutimiza lengo lao.