Uhuru arejea Ikulu ya Kenya

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta (55) amefanikiwa kutetea nafasi yake baada ya kuibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Jumanne wiki hii huku nafasi hiyo ikishirikisha wagombea wanane.

Hata hivyo, mchuano mkali ulikuwa kwa Uhuru na mgombea wa Muungano wa Vyama vya Upinzani (NASA), Raila Odinga (72) ambaye hiyo ilikuwa mara yake ya nne kuwania urais wa nchi hiyo, lakini mara zote ndoto zake zikiishia kwenye sanduku la kura.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa awali kabla ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Uhuru kutangaza matokeo rasmi yalionesha Uhuru kuibuka mshindi kwa kura 8,191,829, sawa na asilimia 54.19, akifuatiwa na Raila aliyepata kura 6,788,734, sawa na asilimia ya 44.9.

Ushindi wa Uhuru umetengeneza tofauti na kura 1,403,095 dhidi ya Raila, Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu uliofanyika katika vituo 40,883, wapigakura milioni 19.6 walijiandikisha.

Hii ni mara ya pili kwa Uhuru kumbwaga Raila, kwani katika mchuano wa mwaka 2013, Uhuru aliibuka mshindi kwa jumla ya kura 6,173,433 sawa na asilimia 50.07 ya kura milioni 12.3 zilizopigwa katika uchaguzi huo ulioshirikisha wagombea wanane wa kiti cha urais na hivyo kutangazwa Rais wa nne wa Kenya akiwa na umri wa miaka 51.

Raila, mwaka 2013 akiwa anatumbukiza kete yake kwa mara ya tatu baada ya kuwa alishindwa katika chaguzi za mwaka 1997 mbele ya Daniel Arap Moi na 2007 mbele ya Mwai Kibaki, alivuna kura 5,340,546 sawa na asilimia 43.3. Ilimaanisha kuwa, mwaka huo Uhuru alimzidi Raila kwa kura 832,887.

Mgombea mwenza wa Uhuru alikuwa William Ruto ambaye ni Naibu Rais wa nchi hiyo. Marais wengine waliowahi kuiongoza Kenya ni Jomo Kenyatta ambaye ni baba mzazi wa Uhuru, Daniel Arap Moi na Mwai Kibaki.

Raila, naye ana harufu ya Ikulu, kwani ni mtoto wa aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa zamani wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga. Wagombea wengine wa urais na kura zao kwenye mabano ni Joseph Nyagah (37,859), Mohammed Abduba Dida (37,326), Dk Ekuru Aukot (27,337), Dk Japhet Kaluyu (11,632), Cyrus Jirongo (11,263) na Michael Wainanina (8,845).

NASA wasusia sherehe Hata hivyo, wagombea wakuu kutoka muungano wa NASA wakiongozwa na Raila na mgombea mwenza wake, Kalonzo Musyoka, walisusia sherehe ya kutangaza matokeo katika kile ambacho msemaji wake, Musalia Mudavadi alisema ni kutokukubaliana na matokeo yaliyompatia ushindi Uhuru.

Pamoja na kuwepo katika ukumbi wa Bomas ambako matokeo hayo yalitangazwa kwa muda mrefu kuanzia asubuhi jana, Mudavadi alisema wameamua kuondoka baada ya kuwasilisha malalamiko yao kwa IEBC na kwamba hata hivyo, tume hiyo ilikataa kusitisha kutangaza matokeo na kuahidi kuwa ingefanyia kazi malalamiko yao baada ya kutangaza matokeo.

Wanawake historia Uchaguzi wa mwaka huu umekuwa wa kihistoria kwa wanawake, baada kung’ara katika ubunge, ugavana na nafasi nyingine katika uchaguzi huo, idadi inayotajwa haikuwahi kutokea siku za nyuma.

Katika Jimbo la Ijara, Kaskazini Mashariki mwa Kenya, Sophia Abi Noor wa chama cha Party of Development and Reforms (PDR) ameshinda katika jimbo hilo, huku mwandishi wa habari wa zamani, Naisula Lesuuda wa KANU akiibuka mshindi katika Jimbo la Samburu Magharibu.

Huko Nakuru katika Jimbo la uko Huko Huko Njoro, Charity Katambi Chepkwony ameibuka mshindi na kuwa mwanamke wa kwanza kushinda ubunge katika jimbo hilo. Wengine na majimbo yao kwenye mabano ni Janet Sitienei (Turbo), Anne Wanjiku (Gatundu Kaskazini).

Gatundu ni mwandishi wa zamani wa kituo cha redio cha Kameme FM. Naye Naibu Spika wa Bunge la Kenya, Joyce Laboso, amekuwa mmoja wa magavana wa kwanza wanamke nchini Kenya baada ya kushinda nafasi hiyo huko Bomet, nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Isaac Ruto wa Chama Cha Mashinani (CCM).

Anne Waiguru wa Jubilee, aliungana na Laboso kwani naye akishinda huko Kirinyaga, akimwangusha Waziri wa zamani, Martha Karua. Katika Kaunti ya Kitui, Waziri wa zamani katika Serikali ya Mwai Kibaki, Charity Ngilu wa NARC ameutwaa Ugavana akimbwaga Julius Malombe.

Aidha, katika Kaunti ya Nandi, Cynthia Jepkosgei Muge, binti mwenye umri wa miaka 24 na msomi wa Chuo Kikuu cha Nairobi, ameibuka mshindi wa kiti cha Udiwani Kilibwoni alikokuwa mgombea binafsi. Naye Nancy Chemutai (26), ameibuka mshindi katika Kata ya Kobujoi.

Wanahabari wang’ara Miongoni mwa washindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni waandishi sita wa habari. Hao ni pamoja na Granton Graham Samboja, mtangazaji wa zamani kituo cha redio cha Jambo aliyechaguliwa kuwa Gavana wa Kaunti ya Taita Taveta kwa tiketi ya chama cha Wiper.

Mwanahabari mwingine machachari kwa habari za uchunguzi, Mohammed Ali aliyejipatia umaarufu kupitia kipindi chake cha Jicho Pevu kwenye runinga, ndiye mbunge mteule wa Jimbo la Nyali. Alijitosa akiwa mgombea binafsi baada ya kushindwa katika kura za maoni kupitia chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

Mwandishi mwingine ni Paul Katana aliyeshinda katika Jimbo la Kaloleni kwa tiketi ya ODM. Mhariri wa zamani wa gazeti la Standard, Enoch Wambua amechaguliwa Seneta wa Kaunti ya Kitui kwa tiketi ya Wiper, huku mtangazaji wa zamani wa Shirika la Utangazaji Kenya (KBC), Josephine Naisula Lesuuda akishinda ubunge katika Jimbo la Samburu Magharibi kwa tiketi ya KANU.

Gathoni Wamuchomba, mtangazami wa zamani wa kituo cha redio cha Kameme FM naye ameibuka mshindi, akitangazwa kuwa Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Kiambu kwa tiketi ya Jubilee.

Mama na mwana Katika Jimbo la Bomet Mashariki, Beatrice Kones aliibuka mshindi dhidi ya mwanaye wa kumzaa, Kipng’etich Kones ambaye ni mtoto wa waziri wa zamani, Kipkalya Kones.

Beatrice wa chama tawala cha Jubilee alipata kura 22,796 dhidi ya 2,410 za mwanaye katika kinyang’anyiro hicho cha ubunge baina ya watu wa familia moja. Kipng’etich aliwania ubunge kupitia Chama Cha Mashinani (CCM) huku akipata sapoti kubwa kutoka kwa mbunge aliyemaliza muda wake, Isaac Ruto.

Mwanafunzi ashinda Mwanafunzi John Mwirigi mwenye umri wa miaka 23 na ambaye alifanya kampeni kwa miguu kutokana na kutokuwa na fedha, ameibuka mshindi wa kiti cha ubunge katika Jimbo la Igembe Kusini. Aliwania ubunge akiwa mgombea binafsi.

Raila na wafungwa Juzi, IEBC ilitangaza matokeo ya kura za wagombea wa nafasi ya urais kwa kura zilizipigwa magerezani na nje ya Kenya. Katika matokeo ya kura zilizopigwa na wafungwa, Raila aling’ara kwa kupata kura 2,048, Uhuru (1,710), Nyagah (9), Dida (7), Aukot (4), Jirongo (2), Japhet Kaluyu (2) na Waura (2). Wakati tunaenda mitamboni, saa 3.30 usiku Mwenyekiti wa Tume alikuwa anaanza kutangaza rasmi matokeo hayo.