Madola wamkubali Shein, Maalim Seif chali kortini

JUMUIYA ya Madola imeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbalimbali za maendeleo kama ilivyo kwa wanachama wengine wote 52 wa Jumiya hiyo.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Patricia Baroness Scotland aliyasema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar jana.

Katika maelezo yake, Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa Jumuiya ya Madola inaendelea kutekeleza mipango na mikakati kabambe ambayo imeiweka kwa wanachama wake ikiwemo Tanzania ambapo Zanzibar pia, ni miongoni mwao.

Scotland alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Rais Dk Shein kwa juhudi kubwa anazozichukua katika kuhakikisha Zanzibar inakuza uchumi na kuimarisha amani na utulivu na kusisitiza kuwa jumuiya anayoiongoza haitokuwa nyuma kumuunga mkono.

Aidha, Scotland alimueleza Dk Shein kuwa miongoni mwa mipango ya jumuiya hiyo kwa nchi wanachama wake wote 52 ni pamoja na kuongeza fursa katika sekta ya biashara na uchumi, kuwasaidia wanawake, vijana, upatikanaji ajira kwa vijana, elimu, kutunza mazingira, uwezeshaji na mengineyo.

Aliongeza kuwa uchumi kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo umekuwa ukiimarika kwa kiasi kikubwa kwa zile nchi za Bara la Afrika na hata nchi za Bara la Asia uchumi wake umeimarika kwa asilimia 5 hadi asilimia 8.

Katika mazungumzo hayo, Scotland alimueleza Dk Shein kuwa miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele na Jumuiya hiyo ni katika kuhakikisha nchi zake wanachama zinaimarika kiuchumi ni pamoja na miundombinu na nishati.

Naye Rais Shein kwa upande wake, alitoa pongezi kwa kiongozi huyo kwa ujio wake hapa Zanzibar sambamba na juhudi kubwa zinazochukuliwa na jumuiya hiyo katika kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Katika hatua nyingine Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi ya Bodi ya CUF inayotambulika na Katibu Mkuu, Maalim Seif Hamad ya kutaka Msajili wa vyama vya siasa asitoe ruzuku kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Katika hatua nyingine Jumuiya ya Madola imeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbalimbali za maendeleo kama ilivyo kwa wanachama wengine wote 52 wa Jumiya hiyo.

Jaji Wilfred Dyansobera aliyatupa maombi hayo namba 21 ya mwaka 2017 baada ya kusema kuwa anakubaliana na moja kati ya mapingamizi ya Mwanasheria wa Mkuu wa Serikali (AG) kwamba vifungu vya sheria vilivyotumika kufungua shauri hilo si sahihi.

Mahakama Kuu kutupilia mbali maombi ya Bodi ya CUF imekuja baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata anayemuwakilisha mdaiwa wa pili ambaye ni AG, kudai kuwa kesi imekuja kwa ajili ya uamuzi.

Katika kesi hiyo ambayo wadaiwa ni Profesa Lipumba na AG, Jaji Dyansobera alisema kuwa licha ya kukubaliana na hoja za upande wa serikali anakubaliana na hoja za Bodi hiyo ya Maalim Seif kwamba suala la bodi kutokuwa na uhalali linahitaji ushahidi wa kina.

Pia kuhusu suala la Maalim Seif kusaini hati mbalimbali za shauri hilo bila kupewa mamlaka, amesema siyo pingamizi kwani mahakama haiwezi kutoa uamuzi kwa kuangalia kiapo tu. Baada ya uamuzi huo, upande wa Maalim Seif umedai kuwa watafungua upya kuhusu suala la ruzuku. Mwandishi Wetu, Zanziba na Francisca Emmanuel, Dar