Waziri Mkuu awaonya wakazi wakimbizi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa (pichani) amewataka wananchi wanaoishi kwenye makazi ya wakimbizi ya Ulyankulu waache kujihusisha na matukio ya uhalifu.

Alitoa onyo hilo jana wakati akiwahutubia mamia ya wakazi wa tarafa ya Ulyankulu katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya VETA, wilayani Kaliua mkoani Tabora.

Alisema matukio ya ujambazi, mauaji na umiliki wa silaha yanayofanyika kwenye tarafa hiyo ni mengi ikilinganishwa hali ilivyo kwenye maeneo mengine ya mkoa huo. “Taarifa nilizonazo zinaonesha katika kipindi cha miaka miwili kumekuwa na matukio ya mauaji 35, ujambazi matukio 12, umiliki wa silaha nao unatisha.

Yamekamatwa magobole 11, bunduki aina ya SMG saba na Mark Four mbili. “Tulikamata pia risasi 714 za SMG zikiwa kwenye ndoo za mafuta na juu yake wamepaka mafuta ya mawese.

Pia risasi mbili za Mark Four zilikamatwa,” alisema Waziri Mkuu. Waziri Mkuu aliwataka wakazi hao ambao baadhi yao wamepewa uraia na wengine bado ni wakimbizi waonyane wanapokutana kwenye vikao vyao kwa sababu matendo yao yanaikwaza Serikali ambayo iliamua kuwapa hifadhi.

“Ni vema mkikutana kwenye vikao vyenu muelezane na kuonyana. Ninawasihi matukio haya myadhibiti la sivyo mtaharibu nia njema iliyoleta uwepo wenu. Bunduki na risasi zinakuja kufanya nini wakati nyie mko maeneo salama? Mauaji ya nini? Kama kuna tatizo limekupata, muone mwenyekiti wa kijiji, atakusaidia,” alisisitiza.

Alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi yao ambao wamegeuka mawakala na wameanza kuwaleta ndugu zao bila kufuata utaratibu. “Hatuzuii mtu kutembelewa na ndugu yake, lakini ni lazima mfuate taratibu. Tunataka tudumishe amani iliyopo nchini lakini pia tudumishe urafiki wa nchi zetu mbili za Burundi na Tanzania,” aliongeza.

Mapema, Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, John Kadutu alimuomba Waziri Mkuu afuatilie suala la upatikanaji wa maji kwenye tarafa hiyo, pia aliomba wasaidiwe ili kata tatu za Kanindo, Igombenkulu na Milambo ziwezeshwe kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.