Jukwaa la Biashara kuiandaa Tanga na fursa za bomba

WIKI ya kuelekea k w e n y e Jukwaa la biashara mkoani Tanga inaanza kesho huku Mkuu wa Mkoa wa huo, Martine Shigela akisema jukwaa hilo litasaidia kuwaandaa wakazi wa mkoa wake kushiriki kikamili kwenye fursa zinazokuja na bomba la mafuta.

Agosti 5, mwaka huu, Rais John Magufuli na mwenzake wa Uganda, Yoweri Museveni waliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba hilo la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga linalotarajiwa kuibua fursa nyingi za uwekezaji, mbali na ajira.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na timu ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Shigela alisema Jukwaa hilo litakalorindima Alhamisi ijayo, Agost 17 mwaka huu, mbali na kuwaandaa wana Tanga kifikra, litatumika pia kutangaza fursa zinazopatikana mkoani humu.

Hili ni jukwaa la tatu kuandaliwa na TSN inayochapisha magazeti ya HabariLeo, Daily News na SpotiLeo. La kwanza lilifanyika Mkoani Simiyu mwezi Februri na la pili likafanyika Mwanza, mwezi Aprili.

Shigela alisema halmashauri zote 11 za mkoa wa Tanga zimetakiwa kutambua vikundi, wafanyabiashara na wawekezaji ambao wana nia ya kuwekeza katika mkoa wa Tanga ili kushiriki kwenye jukwaa hilo.

Alisema halmashauri pia zimetakiwa kuorodhesha fursa zinazopatikana katika maeneo yao ili iwe rahisi kwa wananchi na hususani wawekezaji kuziendea. Fursa hizi pia zitachapishwa katika gazeti hili kupitia toleo maalumu la Mkoa wa Tanga litakalotoka siku hiyo ya Jukwaa, Agosti 17.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga alisema katika Jukwaa hilo, wananchi mbalimbali, hususani wafanyabiashara wadogo na wa kati, watakutana na wataalamu mbalimbali na kujua pale wanapokwama katika kuboresha biashara.

Alisema wafanyabiashara wengi wana nia ya kunufaika na biashara zao lakini wana matatizo madogo madogo kama vile kutojua ni wapi watapata mitaji yenye unafuu, masuala ya usajili, taratibu za kodi na kadhalika ambayo kupitia jukwaa hilo watapata majibu.