Mali za mil 300/- zanadiwa kulipa madeni ya ushirika

MALI mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 300 zimepigwa mnada mkoani Ruvuma ili kulipia madeni yaliyokopwa katika vyama vya ushirika.

Minada hiyo iliyoendeshwa na Kampuni ya Kapondogoro Auction Mart, ilifanyika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu la kukusanya madeni yote na kufufua vyama vya ushirika. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Mathew Mkumbo, vyama vya ushirika Ruvuma vinadai Sh bilioni nne.

Mnada huo ulijumuisha uuzaji wa magari, pikipiki fenicha za ndani pamoja na madeni ya nyuma. Pamoja na kufanya minada katika Mkoa wa Ruvuma, kampuni hiyo imepewa dhamana ya kukusanya zaidi ya Sh bilioni 20 katika mikoa saba ya Tanzania Bara.

Mkumbo alisema vyama vingi vya msingi vimekufa kutokana na wanachama wa vyama hivyo kujenga tabia ya kukopa na kushindwa kurudisha. Alisema wamepewa mamlaka ya kukusanya madeni katika mikoa ya Ruvuma, Iringa, Mwanza, Shinyanga, Lindi, Mtwara na Simiyu.

Mkurugenzi huyo alisema kwa sasa wanakamata vitu walivyoweka rehani wakati wa mikopo. Hata hivyo, alisema wale ambao wamejisalimisha wanatengeneza mpango wa malipo ili vitu vyao visikamatwe.