Diwani Chadema aifagilia serikali

DIWANI wa Kata ya Kabwe mwambao mwa Ziwa Tanganyika, Nkasi mkoani Rukwa, Asante Lugwisha kupitia Chadema, ameifagilia Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwajali wanyonge huku akisisitiza kuwa maendeleo hayana itikadi za chama.

Lugwisha alibainisha hayo alipopewa nafasi ya kusalimia wananchi wakati wa uzinduzi wa mradi kamambe wa kusambaza umeme vijiji awamu ya tatu mkoani Rukwa katika sherehe zilizofanyika katika kijiji hicho kilichopo mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi.

Aidha, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, Ally Kessy alimfagilia Lugwisha kwa kusema kuwa licha ya kuwa anatoka chama cha upinzani, lakini amekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wananchi katika shughuli za maendeleo akitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika sherehe hizo za uzinduzi wa mradi wa REA awamu ya Tatu zilizohudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi, pia alikuwepo Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Kabwe , Christina Isaac.

“Niishukuru Serikali ya Awamu ya Tano, kilio chetu kikubwa kilikuwa umeme katika kata hii ya Kabwe, hakika nisema wazi kuwa maendeleo ni kwa Watanzania wote hayana chama… sisi sote tunahitaji umeme hii ni furasa kubwa sana wetu,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda aliuchekesha umati uliohudhuria alipomweleza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani kuwa Diwani Lugwisha amefurahia sana uzinduzi wa mradi wa REA, kwani ameshona na kuvaa suti mpya ya uzinduzi. Naye Dk Kalemani alimwita jukwaani Lugwisha pamoja na kumwagia sifa lukuki alimweleza, “ni namna tu ya kuingia huku (CCM), lakini njia ipo wazi kwako.”