Ubakaji waitafuna Unguja

SERIKALI ya Mkoa wa Kaskazini Unguja inakabiliwa na kasi ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsi ikiwemo matukio ya ubakaji na mimba kwa wanafunzi.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Vuai Mwinyi wakati akisoma taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini mbele ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein katika ziara ya kuangalia maendeleo ya mkoa huo.

“Tunakabiliwa na matukio ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo ubakaji na mimba kwa wanafunzi wa shule ambapo hata hivyo tumeanza kudhibiti kwa kutoa elimu pamoja na kesi hizo kusikilizwa haraka haraka katika mahakama zilizopo katika mkoa,” alisema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman alisema tayari vyombo vya sheria ikiwemo mahakama na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na jeshi la Polisi wamenza kuzipatia ufumbuzi wa haraka kesi za udhalilishaji wa kijinsia.