Majeruhi Lucky Vincent kurejea Ijumaa

SAFARI iliyoibua majonzi baada ya watoto watatu waliopata ajali ya basi la Shule la Lucky Vicent iliyoua watu 35 na hatimaye watoto watatu wakapona, hivi sasa imekuwa furaha baada ya watoto hao kutarajia kuwasili siku ya Ijumaa kutoka Marekani.

Akizungumza na gazeti hili jana jijini hapa, Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu alisema watoto hao ambao ni Doren Mshana, Sadya Awadh na Wilson Tarimo, wanatarajia kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) wilayani Hai mkoani Kilimanjaro saa tatu asubuhi.

Nyalandu alisema ndugu jamaa na marafiki, watakuwepo uwanjani hapo kuanzia saa 1:00 asubuhi huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye atafika kwa ajili ya kuwapokea watoto hao ambao walikuwa kwenye matibabu nchini Marekani.

Majeruhi hao waliondoka nchini Mei 15, mwaka huu na walitarajiwa kupata matibabu ya kina ya mifupa kutokana na majeraha waliyopata ikiwamo kuvunjika mifupa ya miguu, mkono, taya, shingo na nyonga.

Watoto hao watatu walikwenda nchini Marekani kwa safari ya saa zaidi ya 20 angani wakiwa na ndege ya Shirika la Mfuko wa Msamaria la Marekani, linaloendeshwa na Frankline Graham ambaye ni mtoto wa mhubiri maarufu duniani, Bill Graham.

Ndege hiyo aina ya DC 8 ambayo iliwachukua watoto hao ilikuwa siku ya Jumapili saa 11:45 alfajiri na ilifika Uwanja wa Ndege wa Charlotte Jimbo la North Calorina kisha watoto hao kupanda ndege nyingine ndogo hadi Jimbo la Iowa kwa ajili ya matibabu yao.

Nyalandu alisema siku ya kwanza walipopata ajali Mei 6, mwaka huu hali zao zilikuwa mbaya, lakini wanawashukuru timu nzima ya madaktari kwa moyo wa pekee kwa watoto hao kwani hali zao ni nzuri hivi sasa.

Ajali hiyo iliyotokea Karatu mkoani Arusha, ilipoteza maisha ya watu 35 wakiwamo wanafunzi 32, walimu wawili na dereva. Alisema ndege hiyo iljpofika nchini Marekani, shirika hilo la Msamaria liliandaa ndege nyingine maalumu (Air Ambulance) iliyowabeba uwanjani hapo kwenda katika Hospitali ya Mercy iliyopo Jiji la Sioux lilipo Jimbo la Iowa.

Watoto hao waliambatana na muuguzi na mtaalamu wa wagonjwa mahututi na waliopata ajali kutoka Hospitali ya Mount Meru, Siniphorosa Silalye na daktari bingwa wa Mifupa, Dk Elias Mashallah.

Wakati wakiondoka nchini, ndugu, jamaa na wazazi wa watoto hao, waligubikwa na majonzi, huku baba zao wakishukuru juhudi zilizofanywa kufanikisha safari hiyo. Baba wa Sadia, Awadhi Mohamed alisema anashukuru kwa msaada mkubwa uliotolewa na serikali, wadau mbalimbali na Mfuko wa Samaria kwa kuhakikisha maisha ya watoto wao yanaimarika.

“Natarajia watoto watarudi salama tuzidi kuwaombea,” alisema Mohamed. Kwa upande wake, baba wa Doreen, Elibariki Mshana alisema wana kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kile kilichotokea.

“Tusihukumu katika jambo lolote bali tushukuru kwa kila jambo lililotokea,” alisema Mshana. Naye Baba wa Wilson, Godfrey Tarimo alisema mtoto wake anaendelea vizuri hivyo ana imani atapona.