TRA: Jukwaa la Biashara linasaidia kupata mrejesho

MKURUGENZI wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Richard Kayombo amesema Jukwaa la Biashara linalofanyika hapa kesho lina manufaa makubwa kwa ajili ya kutoa elimu kwa mlipa kodi.

Akizungumza na gazeti hili, Kayombo alisema kupitia Jukwaa la Biashara linaloandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), wamefikisha elimu sahihi ya kodi kwa wananchi na pia kupata mrejesho wa nini kinawakwaza.

Alisema kupitia jukwaa hilo, serikali imesikia kilio cha wananchi kuhusu masuala mbalimbali yanayowakera wananchi ikiwemo kodi ya umiliki wa gari maarufu kama ‘road license’ ambayo serikali imeifuta na sasa kiasi hicho kinalipwa kwenye mafuta.

“Kama utakumbuka, katika jukwaa lililofanyika Simiyu, Mbunge wa Busega, Raphael Chegeni, alihoji kuhusu kodi hiyo na magazeti yenu yakaandika,” alisema Kayombo. Alisema jukwaa la Simiyu pia liliizindua mamlaka hiyo kujua kwamba wananchi katika mkoa huo mpya walikuwa wanapata shida kwa kulazimika kufuata huduma kama za leseni za udereva, na kadi za magari Shinyanga.

Alisema kesho TRA watakuwapo jukwaani ili kutoa elimu zaidi ya kodi na kusikiliza yale yanayowakwaza walipa kodi wa Tanga kwani TRA inasimamia mapato ya serikali.