Ruvuma yaanza kupiga chapa ng’ombe

MKOA wa Ruvuma umezindua mkakati wa utambuzi wa mifugo kwa kuchapa ng’ombe alama zitakazosaidia katika kudhibiti uingiaji holela wa mifugo mkoani humo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa huo, Dk Binilith Mahenge wakati akizungumzia juu ya upigaji marufuku mifugo kuingia mkoani humo ikiwa kama njia ya kuchukua tahadhari ya kuzuka migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima.

Kwa mujibu wake, kazi hiyo inaenda sanjari na utengaji wa maeneo kwa ajili ya mifugo na kuwaagiza wakuu wa wilaya kuendelea kwa nguvu zote ili kuhakikisha hakuna ng’ombe wanaoingia toka mikoa mingine.

Aidha, Dk Mahenge amewaonya watendaji na wevyeviti wa vijiji kuacha kuruhusu kuingiza mifugo katika maeneo yao, badala yake kuisaidia serikali ya mkoa katika mkakati wake wa kutenga ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa amewahamasisha wananchi kuanzisha na kujiunga na vyama vya ushirika kwani umoja wao utajidhihirisha kwa vikundi na vyama vya ushirika vya uzalishaji vilivyopo.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa hadi sasa katika mkoa huo kuna jumla ya vikundi vya ushirika 280 vyenye wanachama 79,907 na mtaji wa Sh 9,404,275,566 idadi ambayo ni ndogo kwa mkoa mkubwa kama Ruvuma.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2016/2017 katika kuwawezesha kiuchumi mikopo iliyotolewa kwa wananchi ilikuwa Sh 25,555,720,535 sawa na asilimia 78.53 ya urejeshaji wa mikopo iliyotolewa.