Wazua vurugu Mbeya, wadhibitiwa

VURUGU kubwa zimezuka kati ya Jeshi la Polisi mkoani Mbeya na wafanyabiashara waliounguliwa katika soko la Sido jijini Mbeya baada ya polisi kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya.

Vurugu hizo zilitokea baada ya wafanyabiashara waliokuwa wakifunga njia wakidai kupewa kibali kuendelea kujenga maduka kwa matofali katika eneo lililoungua licha ya serikali kutaka kusubiri kupisha uchunguzi.

Akiwasihi wafanyabiashara hao wenye jazba, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, William Ntinika alisema ameunda tume ya kufanya tathimini ya uharibifu uliotokea pamoja na kujua chanzo cha moto kisha kutoa mapendekezo tume ambayo itafanya kazi kwa siku tano.

Alisema ni vema wafanyabiashara wakawa wavumilivu na watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati tume inayoongozwa na Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya ikifanya tathmini na kuja na majibu ambayo wafanyabiashara watapewa pamoja na mapendekezo nini kifanyike baada ya kupata majibu.

Hata hivyo pamoja na majibu hayo wafanyabiashara hao walianza kuzomea wakishinikizwa wapewe majibu jana hiyo hiyo ili waendelee kujenga na kudai kuwa hawapo tayari kusubiri ramani na pia watajenga maduka ya kudumu si ya muda mfupi kwa kutumia mbao kama awali.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Nyasebwa Chimagu, aliwataka wafanyabiashara hao kutuma viongozi wao washirikiane na tume ili kufanya tahmini ya pamoja lakini bado walipiga kelele kupinga jambo hilo na kudai wapewe ruhusa au apigiwe Mkuu wa Mkoa ili awape ruhusa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga aliwasihi wafanyabiashara hao kuwa Jeshi la Polisi pia limesikitishwa na tukio la moto hivyo kila mtu arudi nyumbani kuendelea na kazi zake kusubiri maelekezo mengine