Sirro awapa somo waliostaafu jeshini

MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro amewataka askari wanaostaafu kuliwakilisha vyema jeshi hilo wakiwa uraiani pamoja na kushirikiana na wananchi katika masuala ya ulinzi na usalama.

Sirro alitoa kauli hiyo jana wakati wa hafla ya kuwaaga Makamishna watatu wa jeshi hilo ambao wamefikia umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria kwa kutimiza umri wa miaka 60 katika utendaji wao wa kazi.

Makamishna hao ni pamoja na aliyekuwa Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, aliyekuwa Kamishina wa Polisi Zanzibar, Hamdani Omari Makame na aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Kudhibiti|Dawa za Kulevya, Kenneth Kasseke ambaye alishindwa kuhudhuria hafla hiyo kutokana na kuwa katika majukumu mengine ya kikazi.

Alisema askari hao wamelitumikia vizuri jeshi hilo lakini wanapaswa kuwa na mwenendo mwema kwa sababu wananchi wanawaona kama bado ni askari. “Nawapongeza maana kustaafu kwa namna hii ni heshima kubwa ninawaomba mtakapokuwa huko uraiani mkatuwakilishe vyema muhakikishe wananchi wanawaona ni wastaafu lakini bado mna nidhamu ya kijeshi,”alisema Sirro.

Aidha Sirro aliwataka askari hao kushirikiana na wananchi husasani Polisi Jamii katika kuimarisha ulinzi na kuepuka kutumia amri walizokuwa wamezoea wakati wakiwa katika jeshi hilo. Kwa upande wake, Chagonja amewataka askari hao warudi wajitadhimini na wahakikishe wanarudi kwenye maadili.

“Tumefanya kazi kwa muda mrefu sasa ni muda wa kupumzika lakini kwa waliobaki wanapaswa kusimama imara ili kusudi wananchi wakiwaangalia waseme kweli wanafanya kazi nzuri kwa kufuata maadili yao,” alisema Chagonja. Naye Makame aliwataka askari wanaobakia kuendelea kushikamana sababu hapo walipofikia ni kutokana na nguvu za pamoja walizokuwa nazo