Wazazi wazimia Lucky Vicent wakiweka maua

TUKIO la uwekezaji wa mashada ya maua katika mnara wa kumbukumbu wa vifo vya wanafunzi wa Shule ya Lucky Vicent lililofanywa na manusura watatu wa ajali hiyo jana liliamsha upya vilio, simanzi na majonzi na kusababisha baadhi ya wazazi wenye watoto waliofariki katika ajali hiyo kuzimia.

Manusura hao; Wilson Tarimo, Sadya Awadh na Doreen Mshana ambao waliwasili nchini juzi kutoka Marekani walikopelekwa kwa matibabu, jana walifika katika shule yao na kwa mara ya kwanza kupata fursa ya kushuhudia mnara ambao hawakuwahi kuuona shuleni hapo kwani ulijengwa kutokana na vifo vya wanafunzi wenzao huku wao wakiwa mahututi hospitali.

Vilio viliibuka baada ya wanafunzi hao kuanza kuweka mashada ya maua katika mnara huo huku wakilia, na hivyo kuwaambukiza majonzi mashuhuda wengi wao wakiwa wazazi wa wanafunzi waliokufa ambao nao waliangua vilio huku wakiita majina ya watoto wao bila kusikia wakiitika, na kuwafanya baadhi kuzimia na kulazimika kupewa huduma ya kwanza na wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu waliokuwepo shuleni hapo.

Uzuni ulitanda zaidi pale majina ya watoto hao wote waliokufa yalipoanza kutajwa moja baada ya jingine na baadaye walimu wao na hatimaye dereva wao. Hatua hiyo ilisababisha kutokea kwa ugumu wa utekelezaji wa kazi hiyo ya kuweka mashada ya maua lililokwenda sambamba na kuwasha mishumaa kama kumbukizi ya manusura hao kwa wanafunzi wenzao ambao wao walifariki dunia.

Mbali ya watoto hao watatu, kazi hiyo iliwahusisha pia ndugu, jamaa, marafiki na madaktari wakiwemo madaktari bingwa waliosaidia kuokoa maisha yao. Wengine walikuwa ni walimu na wanafunzi mbalimbali.

Kabla ya uwekaji wa mashada na kuwashwa kwa mishumaa, risala mbalimbali zilisomwa ikiwemo ile ya mmoja wa wazazi wa waliopoteza watoto katika ajali hiyo ya basi iliyotokea eneo la Rhotia wilayani Karatu, Roland Mwalyambi ambaye aliwataka wanafunzi wa darasa la saba waliosalia shuleni hapo kusoma kwa bidii ili kuleta matokeo mazuri kama ishara ya kuwafuta machozi wafiwa wote.

Mitihani ya darasa la saba itafanyika nchi nzima mwezi ujao. Aliwasihi pia watoto hao walionusurika popote pale watakapoawaona wazazi wa wanafunzi wenzao waliopoteza maisha kuwaita baba au mama ili kuwafariji kisaikolojia na kuahidi kuwa wazazi wafiwa jukumu lao kubwa litakuwa ni kushirikiana bega kwa bega na watoto hao ili kuhakikisha kuwa wanayafikia malengo yao ya baadaye.

Alisema ingawa wazazi na walezi waliofiwa na watoto bado wana uchungu lakini ni lazima wayakubali yaliyotokea ikiwemo kuwapa moyo watoto wa darasa la saba waliobaki ili waweze kufanya mitihani yao salama.

"Tunawapenda na kuwakaribisha watoto wetu nyie mliotoka Marekani kwa matibabu, haya ni mapenzi ya Mungu basi tunaomba mtufute machozi na mkituona popote pale tuiteni baba au mama, wala msisite maana sisi ni wazazi wenu," alisisitiza.

Mmoja wa watoto wa darasa la saba, Ally Jumanne akisoma risala mbele ya wazazi waliofiwa na wageni wengine waliokuwepo mahali hapo alitoa shukrani kwa serikali ya Tanzania na nchi ya Marekani kwa kuwezesha wenzao hao watatu kupona na hatimaye kurudi tena shuleni wakiwa wenye tabasamu.

Alisema ajali ilipotokea walihuzunika sana kutokana na kuwapoteza wenzao hao, walimu wao na dereva lakini hawakuwa na jinsi bali waliyapokea matokeo hayo ingawa inawapa wakati mgumu na kwamba walifurahi jana kuwaona wenzao watatu waliokuwa ndani ya basi hilo wakirudi huku wakiwa na tabasamu pana usoni.

Alishukuru timu ya madaktari, wauguzi wa Tanzania, wasamaria wema pamoja na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini kwa kuwasaidia kwa hali na mali tangu tukio hilo lilipotokea.

Naye Daktari Bingwa wa Mifupa kutoka Marekani, Dk Steve Meyer alisema ilikuwa ni ajali mbaya sana lakini Mungu ni mwema na ametenda miujiza kupitia kwa watoto hao kwani walipotoka Tanzania kwenda Marekani hawakuwa na furaha.

Alisema wakati wakiwa kwenye matibabu watoto hao walikuwa na sifa zinazotofautiana kwani wakati mtoto Wilson alikuwa akiogopa sana sindano wenzake Sadya na Doreen walikuwa wakimya sana lakini wenye kulalamika mara kwa mara kuwa wameumia.

“Lakini leo Mungu ni mwema watoto hawa wamepona na wamekuja hapa shuleni kuwasalimia na sisi kama Shirika la Samaritan Purse na Kijiji cha Steam tutaangalia uwezekano wa kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto hawa kupata ufadhili kwa masomo,” alisema.

Baadaye watoto hao walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na kuendelea kupewa matibabu na akizungumza na waandishi wa habari Mratibu wa safari ya watoto hao, Lazaro Nyalandu alisema watoto hao wataruhusiwa na madaktari wa hospitali hiyo kwenda majumbani mwao wakati muafaka utakapowadia.

Kuhusu elimu ya watoto hao, Nyalandu alisema wamejadiliana lakini bila kufafanua na nani na kuhusu nini lakini akasema wataendelea na masomo yao ya Kidato cha Kwanza mwakani na watasomeshwa hadi elimu ya juu kadri Mungu atakavyowajalia mahali popote pale ndani na nje ya nchi.