Makonda awabana wakandarasi

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amewataka wakandarasi wanaoomba tenda katika mkoa huo kuhakikisha wanapeleka taarifa za kweli kuhusu kampuni zao.

Makonda alitoa kauli hiyo jana wakati wa kongamano la tathimini ya hali ya miundombinu ya barabara za mkoa huo lililowashirikisha wahandisi, makandarasi, wananchi na viongozi wa wilaya, kata na mitaa.

Alisema ubovu wa barabara nyingi umechangiwa na wakandarasi kutokuwa na uwezo na vitendea kazi kama walivyoorodhesha wakati wanaomba kazi hizo. “Unapeleka taarifa za uongo kuwa una kila kitu lakini kwenye uhalisia hauna vifaa sasa niwaambie toeni taarifa za kweli na si mnaposikia kiongozi anakuja mnakimbilia kuomba vifaa kwenye kampuni nyingine ili muonekane mnavyo vya kutosha,”alisema Makonda.

Aidha, mkuu huyo wa mkoa alimuomba Mratibu wa Wakala wa Barabara za Vijini na Mijini (TARURA), Mkoa wa Dar es Salaam, Lusingi Mashashi kuapa mbele ya wananchi kuwa ataitumikia nafasi yake na kuondoa aibu ya mashimo ya barabara yaliyopo katika mkoa huo.

Baada ya agizo mtendaji huyo aliapa kuwa atasimamia na kuondoa aibu hiyo huku akisisitiza kuwepo kwa ushirikiano kutoka kwa watendaji wa wakala huo na kuwataka kuachana na tabia mbaya zilizokuwepo kabla ikiwemo rushwa. Makonda aliwataka wajumbe wote wa wakala huo kutoka kila wilaya kuapa mbele ya wananchi kuwa watazitumikia nafasi zao