Tundu Lissu azidi kupingwa

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amezidi kupingwa na Watanzania kuhusu kasumba aliyojijengea kushangilia mambo mabaya ya nchi na kupinga yenye manufaa kwa taifa huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikitaja mambo mawili kinayosema kina shaka juu yake.

Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Saad Kusilawe alisema jana kuwa, kitendo cha mwanasiasa huyo wa Upinzani kufurahia kuzuiliwa kwa ndege ya Tanzania aina ya Bombardier Q400 Dash 8 nchini Canada, kinatia shaka kuwa huenda ana matatizo katika ufahamu wa mambo, au ni kibaraka wa makaburu wasiowatakia mema watu weusi.

“Tunashindwa kuelewa huyu mtu ni kibaraka wa taifa gani; Lissu hataki kuona jambo zuri kwa Tanzania; yeye ni mtu wa kufurahia matatizo ya Watanzania. Mtu makini, mzalendo, mwenye akili timamu na ambaye siyo kibaraka, hawezi kufurahia matatizo ya nyumbani kwao; huyu ni mtu wa ajabu,” alisema Kusilawe. Akaongeza, “Sijui huyu ni kibaraka au kaburu wa namna gani maana ukaburu ni hulka siyo rangi.

Wapo makaburu weupe wanaopenda maendeleo ya watu weusi na wapo makaburu weusi wanaopenda mambo mabaya kwa watu weusi. Huyu inawezekana ni kibaraka wa mataifa yasiyoitakia mema Tanzania aliyejificha katika siasa za upinzani yaani hata utu wala uzalendo kwa taifa kabisa.” Alisema CCM mkoani Dar es Salaam inalaani tabia ya Lissu, kufurahia mambo mabaya yanayowakumba Watanzania.

“Mtu wa namna hii Watanzania wamuogope na kumpuuza; kauli na matendo yake ni tata, hayana ladha nzuri; yana ukakasi na yamelenga siku zote kubomoa nchi na kuwaangamiza Watanzania. Huyu hapaswi kuwa kiongozi na hana sifa za uongozi; watu wawe makini kwa kumwepuka na kumpuuza,” aliongeza.

Alisema hata wakati Serikali ya Rais John Magufuli ikishughulikia suala la utoroshaji wa dhahabu kupitia makinikia, Lissu alikuwa mstari wa mbele kuitishia na kuwakatisha tamaa Watanzania, ingawa baadaye aliumbuka baada ya ukweli kubainika na kampuni husika zikaja kuomba radhi na kukubali kulipa.

“Tunamuomba Rais Magufuli na serikali yake kwa jumla wasikate tamaa; CCM na Watanzania waliomwamini na kumchangua wanamuunga mkono. Wasikatishwe tamaa na huyu mtu anyeonekana kuliombea taifa liangamie, taifa lifilisike, taifa lidhulumiwe na anayeliombea taifa liibiwe…,” alisema Kusilawe.

Jana baadhi ya wanazuoni, Dk Benson Bana wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja wa Udsm na Dk Damas Ndumbaro ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), walinukuliwa wakihoji uzalendo wa Lissu kutokana na tabia yake ya kushabikia matatizo ya nchi, badala ya kuwa sehemu ya kutafuta ufumbuzi.