NEC yateua madiwani sita CCM, 5 Chadema

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewateua madiwani wanawake wa Viti Maalumu 12 kwa ajili ya kujaza nafasi za wazi za madiwani kwenye halmashauri mbalimbali Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume hiyo, Ramadhan Kailima (pichani), uteuzi huo umefanywa na NEC baada ya kushauriana na vyama vya siasa husika.

Kailima alisema katika madiwani hao wanawake walioteuliwa, jumla ya madiwani sita ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo watano na Chama cha Wananchi (CUF) mmoja.

Aliwataja madiwani wa CCM walioteuliwa kuwa ni Sophia Msangi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Shahara Nduvaruva (Mwanga), Neema Nyangalilo (Mbarali), Farida Mohamed (Mvomero) na Amina Mbaira (Nanyumbu).

Aidha, madiwani wengine wa Chadema walioteuliwa na tume hiyo ni Janeth Kaaya kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Sara Katanga (Ilala), Ikunda Massawe (Hai), Tumaini Masaki (Siha) na Elizabeth Bayyo (Mbulu).

Pia ilimteua Saida Kiriula (CUF) kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa. Alieleza kuwa uteuzi huo umefanyika baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa ambaye kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, aliitaarifu tume hiyo kuhusu uwepo wa nafasi hizo zilizo.