Mshitakiwa Exim Bank ataka afutiwe kesi

MSHITAKIWA wa kwanza katika kesi inayowakabili washitakiwa 15 wakiwemo 13 waliokuwa wafanyakazi wa Benki ya Exim (T) Tawi la Arusha, Bimel Gondael (37), ameiambia mahakama kuwa mashahidi 37 wa jamhuri waliotoa ushahidi katika mahakama hiyo hakuna aliyesema yeye aliharibu nyaraka za benki hiyo.

Gondael ambaye ni Mtanzania mwenye asili ya Kiasia na alikuwa meneja mzoefu katika benki hiyo tangu 2009 hadi 2012, alidai hayo wakati akiongozwa na wakili wake, Adam Jabir mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha/Arumeru, Deusdedit Kamugisha. Gondael ambaye ni shahidi wa 15 wa upande wa utetezi, alidai kutokana na mashahidi wa jamhuri kutomtaja kuhusika na shitaka hilo, aliomba mahakama kumwachia huru.

Alidai Benki ya Exim haikuwahi kutoa taarifa kuwa ilipata hasara kutokana na wizi uliotokea mwaka 2012 na hakuna shahidi wa benki hiyo aliyesimama katika mahakama hiyo kueleza kuwa benki ilipata hasara au Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) nayo ilipata hasara kutokana na wizi huo.

“Lazima kuwe na taarifa ya kifedha ya kila mwaka ya kuonesha hasara na faida na katika kesi hii lazima taarifa hiyo ya ukaguzi wa ndani au nje ingeletwa hapa mahakamani kuthibitisha hilo lakini halikufanyika. Shitaka hili siyo la kweli dhidi yangu na hakuna shahidi aliyethibitisha kuwa niliharibu nyaraka za Benki ya Exim, hivyo naomba mahakama niachie huru,” alidai Gondael.