Kardinali Pengo akabidhi kisima

KANISA Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam limekabidhi kisima chenye thamani ya Sh milioni 11.8 kwa serikali ili kutatua tatizo la maji katika Mahabusu ya Watoto iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam.

Akiongea katika hafla ya makabidhiano ya kisima hicho jana, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo alisema lengo kuu la mchango wa kanisa katika ujenzi wa kisima hicho ni kuonesha kuwa kanisa haliko mbali na serikali katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa. Alisema Kanisa Katoliki Tanzania linashirikiana na serikali katika juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo bila kujali itikadi za kidini, siasa au kabila ili kusudi wanapotoka kwenye vituo hivyo watambue wamesaidiwa kutokana na mapenzi mema ya kanisa hilo kwa watu wote.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema ujenzi wa kisima hicho utasaidia serikali kupunguza gharama ya kulipia bili ya maji ambayo kwa mwezi mmoja serikali ilikuwa inalipa Sh 400,000 kwa ajili ya gereza hiyo.

Waziri Ummy alisema kutokana na ujenzi wa kisima hicho tatizo la maji limekwisha kwa asilimia 100 kwa sababu kisima hicho kina uwezo wa kuzalisha lita 5,000 kwa saa. Aidha alisema kuwa fedha ambazo zimeokolewa na ujenzi wa kisima hicho, zitatumika kwa ajili ya kuwakatia Bima ya Afya watoto wanaozuiliwa katika vituo hivyo ili kuwahakikishia upatikanaji wa matibabu. Alisema ni muhimu kwa jamii kufahamu kuwa ni mahakama tu ndiyo yenye uwezo wa kutoa amri ya watoto kuhifadhiwa katika mahabusu hiyo na siyo mtu au chombo chochote kingine.

Waziri Ummy alimwambia Kardinali Pengo kuwa hapa nchini kuna mahabusu tano ambazo ni Mahabusu ya Watoto Dar es Salaam (Upanga), Mahabusu ya Watoto Tanga, Mahabusu ya Watoto Moshi, Mahabusu ya Watoto Arusha na Mahabusu ya watoto Mbeya.

Alizitaja huduma zinazotolewa na wizara yake kwa watoto walioko kwenye mahabusu hizo kuwa ziko za aina tatu ambazo ni uhifadhi na utunzaji wa watoto, huduma za maadilisho kwa watoto ambao tayari mahakama imewahukumu, na huduma za kijamii za marekebisho ya tabia kwa watoto waliokinzana na Sheria.

Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni mwakilishi wa watoto na vijana wa Injili mtandaoni, Padre Thimotheo Nyasulu alisema kuwa wameamua kutoa msaada huo baada ya kuona changamoto hiyo, walipotembelea kituo hicho Desemba, 2016 kama sehemu ya matendo ya huruma kwa kanisa.