RC awatema watendaji kwa kutozuia bangi

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ameagizwa kumsimamisha kazi Mtendaji wa Kijiji cha Masalawe pamoja na Mtendaji wa kata ya Luale, tarafa ya Mgeta kwa kushindwa kusimamia majukumu ya kazi zao.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe baada ya kumaliza operesheni maalumu kukabiliana na kilimo cha bangi kilichoshamiri katika eneo hilo. Mashamba ya bangi ya zaidi ya ekari 25 yalikutwa kando kando ya mto Mgeta ambayo yalikuwa yanafanyika kwa njia ya umwagiliaji. Watu kadhaa kutoka vitongoji vya Tagata, Kwa Kododo na Lufuna vilivyopo kijiji cha Masalawe, kata ya Luale, tarafa ya Mgeta, wilayani Mvomero walikamatwa kwa kuhusika na kilimo hicho.

Alisema ni jambo la kushangaza kuona kilimo cha bangi inaendeshwa bila kificho wakati viongozi na Mtendaji wa serikali ya kijiji pamoja na kata ambao wamepewa dhamana ya kusimamia ulinzi, amani na ustawi wa jamii, wameshindwa kuchukua hatua kwa wananchi wenye kulima bangi hadi mkoa kuendesha operesheni ya uteketezaji.

“Katibu Tawala wa wilaya ya Mvomero pamoja na DED (mkurugenzi) nakuagiza uwasimamishe kazi mara moja watendaji hawa wa kijiji cha Masalawe pamoja na wa kata ya Luale, wameshindwa kufichua uhalifu wa kilimo haramu cha bangi,” alisema Dk Kebwe. Pia aliagiza uchunguzi ufanywe kwa viongozi hao wa kijiji na kata kuona kama na wao wanashiriki katika kilimo hicho.

Kwa upande wake Kamishina wa Operesheni wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Mihayo Msikhela, aliwapongeza wananchi wa kijiji cha Masawale kutokana na kuonesha kwao moyo wa uzalendo kujitokeza kwa wingi kushiriki na askari kuteketeza bangi iliyolimwa mashambani. “Sijawahi kuona sehemu nyingine nchini tulikopita kufanya operesheni hizi wananchi kujitokeza kuunga mkono kwa kushirikiana kwenye kazi hii.

Lakini wa eneo hili wamejitokeza kushiriki kwa kusaidiana na askari kuteketeza bangi mashambani, hawa ni watu wema na wanachukizwa na jambo hili na wangekuwa ni waharifu wasingejitokeza,” alisema Mihayo. Wilaya ya Mvomero imeonekana kuongoza kimkoa kwa maeneo yake mengi kuwa vinara kwa kilimo cha bangi katika vijiji vya Kata ya Doma, tarafa ya Mlali, vijiji vya Tarafa ya Mgeta na vijiji vya tarafa ya Mvomero na wilaya nyingine zinazofuatiwa ni Kilosa na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.