Sumaye asema hapingi kupokonywa mashamba

WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema hapingi serikali kuchukua mali za raia ikiwamo mashamba yake, lakini ameshauri sheria kutumika katika hilo.

Aidha, amedai kuwa mashamba aliyonyang’anywa na serikali ni kwa sababu ya visasi vya kisiasa, jambo ambalo serikali imekwisha kulikanusha. Hivi karibuni, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema serikali haifuti umiliki wa mashamba kwa kuonea mtu, itikadi zake za kisiasa, dini, rangi ama kabila, bali inazingatia misingi ya kisheria iliyowekwa kwa wale wote wasiyoyaendeleza kwa miaka mingi ikiwamo kushindwa kulipia kodi ya ardhi iliyowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za ardhi zilizopo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Sumaye ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Pwani, alidai mashamba hayo amekuwa akiyalipia kodi na pia ameyaendeleza.

Sumaye alisema athari alizopata baada ya kunyang’anywa mashamba hayo ni kupoteza mali zake zilizopo katika mashamba na hawezi kuhamisha vitu vyake kwa haraka. Kutokana na hilo, amefungua kesi kupinga hatua za serikali.