Malipo ya maji kabla ya huduma yaja

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo ameziagiza mamlaka za maji nchini kuanzisha mifumo ya malipo ya maji kabla ya huduma ili kujiendesha kibiashara zaidi.

Profesa Mkumbo alitoa agizo hilo juzi mjini hapa wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja kukagua vyanzo vya maji, miundombinu yake na kusikiliza kero mbalimbali za wafanyakazi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) na watumishi wa Bonde la Maji Kanda ya Kati.

Alisema ingawa mfumo huo una gharama kubwa wakati wa kuanzisha lakini una manufaa mengi zaidi mara unapokuwa kwenye uendeshaji. Alisema licha ya mfumo huo kudhibiti wateja wasumbufu ambao huwa hawalipi ankara zao za mwezi kwa wakati, pia husaidia kukomesha malalamiko ya kubambikiwa ankara, udanganyifu wa matumizi ya maji na mteja kuwa na uhakika wa kulipia kiasi anachotumia.

“Baadhi ya wateja wakubwa; hasa mashirika na taasisi za serikali, wamekuwa hawalipi ankara zao za maji za kila mwezi kwa wakati muafaka hivyo kukwamisha juhudi za uendeshaji wa mamlaka nyingi za maji nchini,” alisema Profesa Mkumbo na kuongeza:

“Njia pekee ya kuepukana na wateja wa aina hii ni kuanzisha mfumo wa kulipia maji kabla ya huduma kama ilivyo kwa Shirika la Umeme nchini (Tanesco).” Profesa Mkumbo pia alizitaka mamlaka hizo kuwa wabunifu kwa kujitafutia mapato ya ziada badala ya kusubiri ruzuku kutoka serikalini tu kutokana na ukweli kwamba ruzuku ya serikali ni ndogo.