Bima iwafikie wenye kipato duni Dar

MSTAHIKI Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amesema kuwa ipo haja ya kuangalia ni jinsi gani watu wenye kipato duni na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu wanaweza kufikiwa na kuelimishwa umuhimu wa kuwa na bima ya afya.

Meya Mwita alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati alipokuwa akifungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa kujadili upatikanaji wa huduma za afya kwa makundi maalumu sambamba na ukiwa na lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma hizo kwa watu wenye kipato cha chini.

Meya huyo alieleza kuwa watu wenye kipato cha chini, makundi mbalimbali wanashindwa kuwa na huduma hiyo kutokana na kukosa uhamasishaji na elimu ya kutosha hivyo, akashauri kuwa ni vyema jambo hilo likazingatiwa kwenye maeneo yote.