Mkemia Mkuu ashindwa kuthibitisha mkojo uliopimwa ni wa nani

Mkemia kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Domician Dominic (49) ameshindwa kuithibitishia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kama sampuli ya mkojo alioufanyia uchunguzi ni wa Mfanyabiashara Yusufu Manji au Polisi.

Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo kumtaka shahidi huyo wa tatu wa upande wa mashitaka, kuieleza mahakama kama anatambua mkojo huo ni wa nani.

Akijibu swali hilo, Dominic alieleza mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha kuwa hatambui kama mkojo ni wa Manji au Polisi kwa kuwa hakuwepo msalani wakati sampuli hiyo inatolewa badala yake yeye alitoa kontena na kumpatia Polisi ili Manji aweke sampuli hiyo.

Alidai yeye alipokea sampuli hiyo kutoka kwa Polisi na kuipa namba ya maabara 367/2017. Aidha, alidai uchunguzi wa awali aliougundua katika sampuli hiyo ni kwamba mkojo ulikuwa na kemikali inayoitwa benzodiazepines.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Timon Vitalis, Shahidi huyo alidai kemikali hiyo ni dawa ambazo hutumika kwa ajili ya kupunguza maumivu makali kwa maelekezo ya daktari. Pia alidai katika hatua ya pili ya uchunguzi aliona dawa inayoitwa Morphine yenye chembechembe ya heroine ambayo wakati mwingine hutumika wakati wa upasuaji.

Hata hivyo, mahakama hiyo itatoa uamuzi Ijumaa kama mshitakiwa huyo anakesi ya kujibu au la baada ya upande wa mashitaka kufunga ushahidi wake