Dk Abbasi: Magazeti, Majarida kusajiliwa upya

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi amewataka wamiliki wote wa vyombo vya habari za machapisho yakiwemo magazeti na majarida kusajili upya vyombo hivyo kuanzia leo.

Dk. Abbasi amesema zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kifungu cha 5(e) inayotaka kutolewa upya kwa leseni za machapisho hayo.

Amesema usajili kwa machapisho ya zamani utakoma Oktaba 15 mwaka huu, lakini wanaotaka kusajili machapisho mapya hakuna ukomo. Aidha, aliwakumbusha waandishi wa habari kujiendeleza kielimu kwani sheria mpya inawataka waandishi wa habari kuwa na elimu inayoanzia diploma.

Alisema watakaoshindwa kujiendeleza ndani ya miaka mitano watapoteza sifa ya kuwa waandishi wa habari. Kwa mujibu wa Dk. Abbasi, Sheria ya Huduma ya Habari inataka vyombo vya habari kutoka kuwa Tasnia ya habari na kuwa Taaluma.