DC akamata magari yanayojaza abiria

MKUU wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Lydia Bupilipili ameendesha kazi ya kukamata magari ya abiria yanayopakia abiria kuzidi uwezo na kuhatarisha maisha ya abiria hao.

Alifanya kazi hiyo ya kushitukiza juzi kwa nyakati na maeneo tofauti katika barabara kuu ya Bunda, Kisorya hadi Ukerewe mkoani Mwanza. Katika kazi hiyo, mkuu huyo wa Wilaya, alikamata magari matatu yaliyokuwa yamebeba abiria kuzidi uwezo wake na kuyapeleka polisi, huku madereva wa magari hayo wakiswekwa ndani na kupigwa faini kwa mujibu wa sheria.

Akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Bupilipili amekamata magari matatu ambayo ni aina ya Noah yenye namba za usajili T752 DBU, iliyokuwa inaendeshwa na Idd Salum na Noah yenye namba za usajili T703 BVL, iliyokuwa inaendeshwa na Wambura Boniphace, ambazo hufanya safari zake kati ya mjini Bunda na Karukekere wilayani hapa.

Aidha, gari nyingine aliyoikamata ni Toyota maarufu kwa jina la mchomko yenye namba za usajili T 567 CCT, iliyokuwa inaendeshwa na Shani Mzuberi, ambayo hufanya safari zake kati ya mjini Bunda na kijiji cha Guta wilayani hapa.