Chadema yawashukuru wote waliomchangia Lissu

CAHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewashukuru watu wote ambao wametoa michango yao kusaidia matibabu ya Tundu Lissu ambapo mpaka sasa zimepatikana Sh milioni 19.4. Kimesema hali ya mwanasheria wake huyo ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu inaendelea kuimarika taratibu.

Akielezea hali yake kwa masikitiko leo, Katibu Mkuu wa Chadema, Vicent Mashinji amesema hali yake juzi mchana ilikuwa mbaya ambapo ililazimu kumsaidia kupumua kwa kutumia mashine lakini baadaye hali yake iliimarika.

"Hiyo ndio hali ya Lissu, jana hali ikua mbaya ikabidi awekewe mashine ya kupumulia lakini mchana hali ikaimarika wakatoa mashine na asubuhi leo ameamka vizuri anaendelea kupigania pumzi yake," amesema Mashinji.

Mashinji amesema jana saa nne asubuhi alianza kupata matatizo ya kifua ambayo pengine yalitokana na kulala muda mrefu. Mashinji amesema mpaka jana ambayo ni siku ya tano tayari Lissu ameshafanyiwa zaidi ya upasuaji tatu na kwamba imebidi kusitisha upasuaji ili mwili upumzike.

Amesema kwa sasa matibabu yanayoendelea kwa Lissu ni sehemu za ndani ya mwili ambazo zingehatarisha afya yake na kwamba sasa wataanza kushughulikia viungo vya nje. Chama hicho kimewashukuru watu wote ambao wametoa michango yao kusaidia matibabu ya Lissu ambapo mpaka sasa zimepatikana Sh milioni 19.4.