Tume ya Mufti yakabidhi ripoti ya mali za Bakwata

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amekutana na Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu Abubakar Zubeir pamoja ujumbe wake wa Tume ya Mufti iliyoundwa kuhakikisha kwamba mali za Waislamu zinazomilikiwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) zinarejeshwa.

Lukuvi amepokea ripoti hiyo ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kumtaka Waziri wa Ardhi afuatilie kwa makini maeneo yote ya Waislamu yanayomilikiwa na Bakwata na yaliyomilikishwa watu kinyume cha utaratibu yanatafutiwa ufumbuzi.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara, katika ujumbe huo, Mufti ameongozana na Kaimu Katibu Mkuu wa Bakwata, Mwalimu Salim Abeid, Mjumbe wa Baraza la Ulamaa, Shehe Ally Ngeruko, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mufti na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa, Shehe Issa Othman Issa na Katibu wa Tume ya Mufti, Alhaj Omary Igge.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa baada ya kukabidhi ripoti hyo, Mufti Zubeir alimshukuru Waziri William Lukuvi kwa kupokea ujumbe wake wa Tume ya Mufti na kumuomba achunguze na kuchambua kwa makini maeneo yote ya Bakwata yanayohusiana na migogoro ya ardhi.

Tume ya Mufti ya kuhusu urejeshaji wa mali za Waislamu iliundwa na Mufti Zubeir baada ya kukutana Rais Magufuli na kumuomba awasaidie kuhakikisha kwamba mali za Waislamu zinazomilikiwa na Bakwata zinarejeshwa kwa baraza hilo.

Baada ya kupokea ripoti hiyo, Lukuvi amemuahidi Mufti Zubeir kwamba atatekeleza agizo hilo la Rais na ataifanya kazi hiyo katika muda mfupi ujao na kusimamia kikamilifu kwa kufuata sheria.

Mufti aliunda tume hiyo ya watu wanane Agosti mwaka jana na kuipa majukumu makuu sita, ikiwamo kufuatilia mikataba yote ya uuzaji wa viwanja na mali mbalimbali za baraza na taasisi zake nchi zima sanjali na kuona uhalali wa umiliki huo.

Tume hiyo ameiunda kwa mujibu wa Katiba ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kipengele 82 (3) b. Wajumbe wake ni Mwenyekiti Shehe Abuubakar Khalid, wajumbe wengine ni Shehe Issa Othman ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti, Mwalimu Salim Abeid (Katibu) na wajumbe ni Shehe Khamis Mattaka, Ustaadh Tabu Kawambwa, Mwalimu Ally Abdallah, Alhaj Omar Igge na Shehe Mohamed Khamis.

Mbali na kufuatilia mikataba, tume hiyo ilipewa jukumu la kufuatilia suala la misamaha ya kodi mbalimbali zilizoombwa na baraza na taasisi zake nchi zima. Pili ilipewa jukumu la kufuatilia mikataba yote ambayo Bakwata na taasisi zake nchi zima, zimeingia na wapangaji mbalimbali katika maeneo yanayomilikiwa na baraza na taasisi zake.

Mufti huyo alisema tume hiyo itafuatilia mali zote za baraza nchi nzima na kuona hali ya usajili wa mali hizo. Juni mwaka jana akihutubia katika Baraza la Idd el Fitr, Rais Magufuli alitangaza vita dhidi ya viongozi wa serikali na wawekezaji wanaofanya dhuluma na kuchukua mali za madhehebu ya dini nchini.

Alisema viongozi hao wamekuwa wakiwahadaa viongozi wa dini na kisha kuingia nao mkataba ya kitapeli na baadaye wanadhulumu mali za taasisi. Rais Magufuli aliahidi kwamba serikali yake itashirikiana na viongozi wa dini katika kuzikomboa mali zao.