Zitto, Kubenea kitanzini

WABUNGE wawili wa vyama vya upinzani vya Chadema na ACT-Wazalendo wameitwa mbele ya kamati mbili za Kudumu za Bunge kujieleza kuhusu udhalilishaji wa kiti cha Spika na Bunge, huku wakitakiwa kutafutwa popote walipo na kufikishwa mbele ya Bunge.

Wabunge hao ni Mbunge wa Ubungo kupitia Chadema, Saed Kubenea na Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto wa ACT Wazalendo. Ingawa uharaka wa kuitikia mwito umepishana kwa mujibu wa tafsiri ya maagizo ya Spika Job Ndugai, Kubenea leo anatakiwa kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajab (CCM).

Kwa mujibu wa agizo la Kiti cha Spika, mbunge huyo anatakiwa kutafutwa kwa namna yoyote ile hadi afikishwe katika kamati hiyo ili ahojiwe kuhusu kauli aliyoitoa ya kumtuhumu Spika wa Bunge, Job Ndugai kwamba amedanganya kuhusu idadi ya risasi alizopigwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Septemba 7, mwaka huu.

Kwa mujibu wa agizo la Spika, mbunge huyo atafutwe popote pale alipo na kufikishwa leo katika kamati hiyo kabla hajafikishwa katika Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kumuita Spika muongo. Kamati hiyo inaongozwa na Mbunge wa Newala, George Mkuchika (CCM).

“Kumekuwa na upotoshaji mkubwa unaofanywa na Kubenea mara kadhaa ambao unalifedhehesha Bunge na mimi. Naagiza Kamati ya Adadi (Rajab - Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama) imuite na asaidie kamati yeye anafahamu Tundu Lissu alipigwa risasi ngapi,” alieleza Spika Ndugai.

Alisema maneno ya Kubenea aliyoyatoa kanisani tena mbele ya madhabahu yanalilidhalilisha Bunge na kumfedhehesha yeye. Spika Ndugai alikumbusha kwamba ukiwa mbele ya madhabahu ni vyema ukasema ukweli na vitabu vyote vinahimiza ukweli.

Alisema katika maelezo yake bungeni wakati akifafanua amri yake kwamba maelezo aliyoyatoa bungeni kuhusu tukio hilo upande wa idadi ya risasi zilizopigwa alinukuu taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma. “Ukinituhumu nimedanganya unajua zaidi, huyu atawasaidia, muiteni haraka katika Kamati ya Adadi.

Katibu atafutwe aletwe kesho (leo) kwa haraka kwa utaratibu wowote,” alisema na kuongeza kuwa mbunge huyo wa Ubungo apelekwe katika Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kumwita Spika mwongo.

Lissu alijeruhiwa Septemba 7, mwaka huu, nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na sasa anaendelea na matibabu katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya. Aidha, Spika Ndugai aliagiza Zitto kupelekwa katika Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa tuhuma za kutamka kuwa Bunge limewekwa mfukoni na mhimili fulani, wakati wa kukabidhi ripoti mbili za Kamati Teule za Bunge kuhusu rasilimali za madini ya almasi na tanzanite.

“Apate nafasi ya kusikilizwa huko, akahojiwe kuhusu kauli yake kuwa Bunge limewekwa mfukoni na mhimili fulani,” alieleza Spika na kueleza kuwa wabunge wanapaswa kuelewa matamshi na matamko yao na kuelewa kinachoendelea katika Bunge kabla ya kuropoka chochote.

Alisema aliwasilisha ripoti hiyo serikalini kutokana na mfumo wa kamati yenyewe na kuongeza kuwa ripoti za kamati ambazo huwasilishwa ndani ya Bunge ni zile zilizotokana na azimio la wabunge ndani ya Bunge.

“Ni lini imetolewa hoja ya kuundwa kwa kamati? Ni lini mlihojiwa hapa hadi nikazuia kuleta hapa ripoti? Anaitwa nani mbunge aliyeleta hoja? Spika niliona busara kuunda kamati ambazo zitaishauri serikali,” alisema Ndugai huku akimchongea mbunge huyo kwa wapiga kura wake akisema mbunge wao mtoro kwani Spika hana taarifa.

Akizungumzia hatua hiyo ya Spika, Zitto katika akaunti yake ya Twitter alithibitisha kwamba atakwenda mbele ya Kamati ya Maadili, akisema, “Spika Ndugai anajua ninavyomheshimu.