Wachina 5 wakamatwa na magamba 652 ya kakakuona

RAIA watano wenye asili ya China wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma baada ya kupatikana na nyara za serikali kinyume cha sheria.

Watuhumiwa hao walipatikana wakiwa na magamba 652 ya kakakuona na kucha tano kakakuona, kucha nne za simba na jino moja la simba. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muruto akizungumza na vyombo vya habari jana, alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika Kiwanda cha Kusaga Kokoto cha Kampuni ya Sands Industries Limited kilichopo katika Kijiji cha Mpamantwa wilayani Bahi mkoani Dodoma.

Kamanda Muruto alisema watu hao walikamatwa Septemba 11, mwaka huu kwa ushirikiano baina ya Polisi Dodoma na askari wa Kikosi cha Kupambana Dhidi ya Ujangili (KDU) Kanda ya Kati, Manyoni. Kamanda Muruto alisema uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini mtandao wa ujangili na wa wageni wanaoingia nchini ambao wanajihusisha na uhalifu wa aina mbalimbali.

Upelelezi ukikamilika watafikiwa mahakamani kwa mujibu wa sheria. Katika tukio lingine, Kamanda Muroto alisema katika msako unaoendelea katika maeneo mbalimbali mkoani Dodoma, wamewakamata watuhumiwa 12 wa makosa ya kuvunja na kuiba vitu mbalimbali. Alisema licha ya kukamata watuhumiwa hao, pia jeshi hilo limeokoa mali zilizoibwa kutokana na uvunjaji wa nyumba za watu mbalimbali. Alizitaja mali hizo waliokamata kuwa ni televisheni zenye kioo bapa (13), redio sabwoofer mbili, spika tano na deki moja, printa ya kompyuta moja, busta ya gari moja na bhangi kete 12.

Kamanda wa Polisi, Muroto aliwaka wale wote ambao wameibiwa vifaa hivyo katika maeneo mbalimbali wafike Polisi Dodoma ili uzitambua mali zao. Alisema kati ya watuhumiwa hao waliokamatwa ni Dotto Kapenga (43), mkazi wa Chang’ombe, mjini Dodoma ambaye alikamatwa na sare za jeshi zikiwamo kombati, suruali moja, sweta mbili, mikanda mitatu, kofia tano, buti pea moja vyote mali ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Alisema mtuhumiwa huyo pia alikamatwa na koti la mvua na cheo cha luteni ussu ambacho ni cheo kinachomtambulisha askari mwenye nyota moja. “Uporaji wa mali za watu kwa kutumia pikipiki na unyang’anyi wa pikipiki, umepungua hasa baada ya kuwakamata watuhumiwa halisi na kuwafikisha mahakamani. Kamanda Muroto aliwataka wananchi waendelee kutoa taarifa za wahalifu kwa Jeshi la Polisi na wao watazifanyia kazi kwa ukamilifu.