Ummy akiri uhaba taulo za kike

KUMEKUWA na changamoto ya upatikanaji wa taulo za kike katika maeneo ya vijijini hali inayosababisha baadhi ya wasichana na wanawake kushindwa kuzipata.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (pichani) alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Ikupa Alex (CCM). Ikupa alitaka kujua ni lini serikali itakamilisha mchakato wa kupatikana kwa taulo za kike kwa wanawake na wasichana wa vijijini ambao wanapata taabu kuzipata na hata zikipatikana zinakuwa bei ghali.

Waziri Ummy alisema, ni kweli wanawake na wasichana wa vijijini wamekuwa na changamoto ya kuzipata taulo za kike na wakati mwingine hata zikipatikana zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya juu. Alisema katika hali hiyo, wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari, wamekuwa wakikosa masomo kwa siku tatu hadi tano wanapokuwa kwenye hedhi. Ummy alisema tayari wizara yake imeandika barua kwenda Wizara ya Fedha na Mipango kuomba kodi ya taulo za kike iondolewe na akaahidi kuendelea kufuatilia ili kuhakikisha kodi hiyo inaondolewa.

Akijibu swali la msingi la Mbunge Ikupa, aliyetaka kujua serikali inaonaje kuondoa kodi kwenye taulo za kike nchini. Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangallah alisema maombi ya kuondoa kodi hiyo kwenye taulo za kike yamewahi kuwasilishwa na watumiaji na wauzaji wa bidhaa hiyo. “Uamuzi wa suala hilo ulichelewa baada ya kubaini kuwa bidhaa hiyo haikuwa miongoni mwa orodha ya vifaa vya matibabu ambavyo huondolewa kodi isipokuwa zimeondolewa tu ushuru wa uingizaji na aina nyingine za kodi zinazolipwa kama bidhaa nyingine,” alisema.