Jaji Mkuu awabana majaji

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma aliyeteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo, ameanza kazi kwa kutoa rai kwa majaji wafawidhi katika mahakama mbalimbali nchini kumaliza kesi zilizochukua muda mrefu ifikapo Desemba 15, mwaka huu.

Aidha, amewataka majaji hao kuachana na matumizi ya kuandika mienendo ya kesi kwenye makaratasi badala yake waanze kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) itakayowezesha kuendana na kasi ya teknolojia ikiwemo kujua mienendo ya kesi inavyokwenda kutokana na mfumo huo.

Jaji Profesa Juma aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa kufunga kikao cha kiutendaji na kukumbushana majukumu ya kukamilisha kesi za aina kwa wakati. Alisema wananchi wanahitaji haki ikiwemo kesi wanazokata rufaa ili ziishe kwa haraka na kupata nakala za hukumu hivyo ni vyema sasa majaji hao wakajipanga kumaliza kesi mbalimbali kwa muda uliopangwa ikiwemo ili kuondoa usumbufu kwa watu wanaohitaji haki zao za kisheria kwa sababu ya kukosekana kwa jaji.

Jaji Profesa Juma aliyeapishwa wiki iliyopita kushika wadhifa huo, alisema endapo jaji atakuwa ametoka eneo la kazi kwenda sehemu nyingine, ni vyema akawa amemaliza kesi au kutoa taarifa kwa Msajili wa Mahakama ili wananchi waondokane na kukosa haki kutokana na kesi zao kuahirishwa mara kwa mara kwa sababu tu jaji hujamaliza kuandika hukumu.

Alisema ni vyema sasa majaji wakaamua kesi za wananchi ingawa kuna changamoto kubwa ya kesi zenye maslahi kwa nchi kama vile mabenki au viwanda, lakini sasa wanapaswa kuangalia zipi ni muhimu kwa maslahi ya watu wote.

“Lakini pia mnapaswa kusoma kila wakati maana sheria zinabadilika na mwezi Novemba mwaka huu sheria inayohusu dawa za kulevya inabadilishwa sasa endapo sheria hiyo ikibadilishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lazima mjipange kuhakikisha mnashughulikia kesi hizo za madawa ya kulevya.

“Ninyi ni viongozi mnajua kila kitu cha mahakama lazima muwe viongozi wa mfano msipende kujadili masuala ambayo hayafai, tujifunze sasa mabadiliko ya Tehama na kujali afya zenu kwa sababu mnakaa muda mrefu kusikiliza kesi, hivyo naomba tuhakikishe kesi hizi zinaishia kwa muda tuliojipangia,” alieleza Jaji Mkuu.

Awali, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanzania, Ferdinand Wambali alitoa rai kwa majaji hao wanaposafiri kutoa taarifa kwa Msajili wa Mahakama ili kuondoa malalamiko kwa wananchi wanafuatilia kesi zao mahakamani.

Jaji Wambali alisema hivi sasa kuna jumla ya mashauri 2,198 ambayo yamekaa muda mrefu katika mahakama mbalimbali Tanzania huku mashauri 247 yakiwa ni ya zaidi ya miaka mitano hadi 10 na mashauri mengine 10 yakiwa yamezidi miaka 10.

Hivyo alisisitiza majaji hao wafawidhi kutoka kanda mbalimbali kuhakikisha wakajipanga kumaliza kesi hizo sanjari na kuhakikisha kesi za uhujumu uchumi pamoja na kesi nyingine wanazimaliza mapema ili kuondoa changamoto kwa watu wanaohitaji haki mahakamani.