Katibu CCM akerwa na siasa za kuchafuana

KATIBU wa Wilaya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salum Kalli amewataka wananchi kutokuwa na dhana potofu kuwa serikali inahusika katika suala la kujeruhiwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, na wanaowaza hivyo huo ni ushamba wa kisiasa.

Kalli alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na Jumuiya ya Wazazi wa Kata ya Mburahati na kuwausia kutojiingiza katika kauli hizo kwa kuwa serikali haiwezi kujiingiza katika suala la aina hiyo.

Alisema ikumbukwe kuwa Lissu ni mwanasheria maarufu na ni vyema kujiuliza kuwa ni kesi ngapi anazozifanyia kazi akiwa tayari amechukua fedha na hajaweza kuzimaliza kutokana na majukumu mbalimbali.

“Acheni ushamba, wenyeviti wetu wa CCM wangapi waliuliwa huko Kibiti na hakuna mwanachama hata mmoja aliyehusisha mauaji hayo na chama kingine kuhusika na mauaji hayo?” Alihoji Kalli.

Alisema ni vyema kufanya siasa zilizo safi zisiwe za kuchafuana na pindi inapotokea tukio kuviacha vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi yake kwa ajili ya kubaini wanaohusika badala ya kuwaeleza wananchi kauli zisizokuwa na ukweli wowote.

Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Mbunge wa Singida Mashariki, alijeruhiwa kwa risasi mkoani Dodoma, Septemba 7, mwaka huu wakati akielekea nyumbani kwake eneo la Area D mkoani humo wakati akitokea bungeni kwenda kupata chakula cha mchana.

Alipatiwa matibabu ikiwamo upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kabla ya kusafirishwa siku hiyohiyo kupelekwa Nairobi nchini Kenya ambako anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari siku chache baada ya tukio hilo kwamba jeshi hilo limetangaza vita kali dhidi ya watu waliomjeruhi kwa risasi Lissu na imepeleka kikosi maalumu ili kuwasaka wahusika kwa udi na uvumba. Hata hivyo, Sirro alisisitiza ukamataji wa watuhumiwa hao, utafanikiwa zaidi kama wananchi watatoa ushirikiano kwa Polisi kuwezesha wahusika kunaswa kwa haraka