Ajali yaua Watanzania 16 Uganda

WATU 16 raia wa Tanzania wameripotiwa kufa huku wengine saba wakijeruhiwa katika ajali iliyohusisha lori aina ya Mitsubishi Fuso na basi dogo la abiria walilokuwa wanasafi ria Watanzania hao kutoka Kampala, Uganda walikohudhuria harusi ya ndugu yao mwishoni mwa wiki.

Idadi hiyo ni kwa mujibu wa gazeti la New Vision kufikia jana jioni, ingawa taarifa za awali kutoka ubalozi wa Tanzania nchini Uganda na hata katika taarifa ya salamu za rambirambi za Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli kwa wafiwa zimetaja idadi ya waliopoteza maisha kuwa ni 13.

Waliopata ajali hiyo walikuwa wakirejea Tanzania kwa basi dogo la kukodi aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili T 540 DLC, baada ya kuhudhuria harusi baina ya daktari binti wa Kitanzania, Dk Annette Teu Ibingira na mumewe, Dk Treasuer Ibingira, raia wa Uganda.

Chanzo chetu cha habari kinasema maharusi, wote ni madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, jijini Mwanza. Walioana Jumamosi iliyopita jijini Kampala. Bwana harusi ni mtoto wa msomi maarufu nchini Uganda, Profesa Charles Ibingira wakati bibi harusi ni mtoto wa Naibu Waziri wa zamani wa Fedha na baadaye Wizara ya Viwanda na Biashara, Gregory Teu ambaye ni mbunge wa zamani wa Jimbo la Mpwapwa mkoani Dodoma.

Miongoni mwa waliotajwa kupoteza maisha katika ajali hiyo ni pamoja na ndugu sita wa karibu wa Naibu waziri huyo wa zamani ambao ni pamoja na baba yake mzazi, Mzee George Teu.

Wengine ni binti wa Teu ambaye ni mdogo wa bibi harusi, dada wawili wa naibu waziri huyo wa zamani na baba zake wadogo wawili. Lakini pia inaelezwa Mama Mchungaji wa Kanisa Anglikana la Vinghawe wilayani Mpwapwa.

Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa gazeti la New Vision, ajali hiyo ilitokea juzi saa 2 usiku katika eneo la Katonga, wilayani Mpigi katika barabara kuu ya Kampala-Masaka. Imeelezwa kuwa, chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa lori aina ya Mitsubishi-Fusso lenye namba za usajili UAH 970P lililokwenda kuligonga basi dogo.

Naibu Msemaji wa Polisi nchini Uganda, Polly Namaye amesema majeruhi wa ajali hiyo iliyotokea juzi saa 2 usiku, walikimbizwa hospitali ya Nkozi kabla ya kuhamishiwa Mulago, jijini Kampala. Miili ya marehemu ilipelekwa Mulago na baadaye kwenda kuhifadhiwa Hospitali ya Gombe.

Naye Naibu Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Elibariki Nderimo Maleko amekaririwa akisema umehuzunishwa na ajali iliyosababisha vifo na majeruhi na kwamba ubalozi ulikuwa unafuatilia taarifa zaidi juu ya tukio hilo ili kupata idadi kamili ya waliokufa na majina yao.

Katika kufuatilia zaidi tukio hilo, Naibu Balozi Maleko amefuatana na Mwambata katika Ubalozi wa Tanzania nchini humo, Brigedia Jenerali S. Makona. SALAMU ZA MAGUFULI Katika salamu zake za rambirambi jana, Rais Magufuli ameungana na Watanzania na wanafamilia kuwalilia ndugu waliopoteza maisha katika ajali hiyo huku akiwatakia afya njema majeruhi katika ajali hiyo.

Aidha, Rais Magufuli amewataka wanafamilia kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokwa na wapendwa wao na watu muhimu waliowategemea.

Taarifa zaidi zinasema taratibu za mazishi zinaendelea kufanyika na kwamba msiba upo nyumbani kwa Teu, Masaki jijini Dar es Salaam. WALIOKUFA Wakati tunakwenda mitamboni, majina ya waliothibitika kufa wametajwa kuwa ni Sakazi Teu, Mazengo George Teu, Alfred Teu, Esther Teu, Rehema Teu, Happy Soka, Einoth Laizer, Vivian Mchaki, Edwin Kimaryo, Bonny Njenga, Aristarick Shayo. Mwingine, Digna ametajwa kwa jina moja na mwingine ametajwa kuwa ni Shangazi.