Atumia fedha za mkopo kuandika kitabu

MWANAFUNZI wa mwaka wa pili Chuo Kikuu Dar es Salaam(UDSM), Sylivia Sostenes (24) anayesomea Shahada ya Saikolojia ameandika kitabu cha kurasa 47 kwa kutumia fedha za mkopo wa chuo na atakapokamilisha taratibu zinazostahili atakiweka sokoni.

Ni nadra wanafunzi wa chuo kuandika kitabu na hasa ikizingatiwa kuwa kwa mwanadada huyu aliamua kubana matumizi ili atumie fedha za mkopo kuandikia kitabu.

Akizungumza na gazeti hili kuhusu kitabu hicho kiitwacho Mapinduzi ya Mwota Ndoto, alisema, haikuwa kazi rahisi lakini hatimaye amefanikisha azma yake ya kuielimisha jamii namna ya kuwawezesha watoto kutimiza ndoto zao.

Alisema, alikuwa akitenga Sh 100,000 katika kila awamu ya mkopo wa chuo ulipokuwa ukitoka na kwa kuwa mwaka hutoka mara nne hivyo alijikuta akipata 400,000 na akafanikisha kitabu hicho Juni mwaka huu.

Alisema wazo la kuandika kitabu hicho limetokana na marafiki zake wengi aliosoma nao Sekondari ya Lumala mkoani Mwanza ambao walishindwa kutimiza ndoto zao kutokana na kutosikilizwa na wazazi na walezi wao.