Bomoabomoa yazua vurugu Jangwani

WANANCHI waliokuwa wakiishi kinyume na utaratibu kwenye Bonde la Jangwani jana walijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kupambana na jeshi la polisi kuzuia bomoabomoa ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Jiji katika eneo hilo.

Katika mapambano hayo ambayo jeshi la Polisi liliweza kutuliza hali ya vurugu, gari la mwendo kasi pamoja na daladala zilivunjwa vioo kutokana na mawe waliyokuwa wakirusha, lakini pia askari watano wakiwamo wawili wa jiji na watatu wa Jeshi la Polisi walijeruhiwa. Hadi Polisi wanadhibiti vurugu hizo, wakazi hao walisababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo kwa zaidi ya saa tatu kuanzia saa tatu asubuhi.

Kwa mujibu wa mwandishi wetu aliyekuwa kwenye eneo la tukio, alisema kuwa bomoabomoa ilianza saa 3:00 asubuhi lakini wananchi hawakukubali na kuanza kuwarushia mawe na chupa askari wa Jiji ambao walikuwa wanasimamia kazi hiyo. Ilipofika saa 5:00 asubuhi, askari wa jeshi la polisi kwa ajili ya kutuliza ghasia waliwasili ndani ya saa moja na kuweza kudhibiti vurugu hizo kwa kuwatawanya watu hao. Katika mapambano hayo, jeshi la polisi lilifanikiwa kuwakamata baadhi ya watu na kuwapakiza katika gari maalumu lililokuwa limewekwa katika eneo hilo.